Home » » Magufuli aibukia Rufiji, atoa miezi mitano kwa mkandarasi kukamilisha km 17 za barabara ya Ndundu-Somanga

Magufuli aibukia Rufiji, atoa miezi mitano kwa mkandarasi kukamilisha km 17 za barabara ya Ndundu-Somanga

WAZIRI wa Ujenzi John Magufuli ametoa muda wa miezi mitano kuanzia sasa kwa kampuni ya M.A Kharafi and Sons kukamilisha ujenzi wa barabara kuu ya Ndundu Somanga km 57 kwa kumalizia ujenzi katika kipande kilichobakia chenye urefu wa km 17 na endapo itashindwa kukamilisha kwa muda huo basi wafukuzwe kazi.

Magufuli amewataka watendaji wakuu wa wakala wa barabara nchini TANROADS makao makuu, mkoa wa Pwani na Lindi kufuatilia utekelezaji wa agizo hilo ikiwa ni pamoja na kufatilia utendaji kazi wa mkandarasi na mkandarasi mshauri wa kampuni hiyo na katika kipindi cha siku tano hado kumi kama wataonekana hawatoshi basi wafukuzwe kazi mara moja.

Waziri huyo wa Ujenzi amefikia hatua hiyo leo Julai 16 wilayani Rufiji alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo kuu ambayo ni tegemeo kubwa la wakazi wa mikoa ya Lindi na Mtwara ambapo alikuta zoezi la ujezi likifanyika kwa kasi ya chini huku Serikali ikiwa imeshamlipa kandarasi wa ujenzi huo zaidi ya asilimia 90 ya fedha za mradi huo.

Wakati wa ukaguzi wa barabara hiyo, Magufuli alikutana na umati mkubwa wa watu kwenye kijiji cha Malendego Mpakani na Muhoro ambapo walitaka kukutana na Waziri huyo uso kwa uso huku wengine wakitaka kumueleza kilio chao cha uchelewaji kukamilika barabara hiyo hivyo ilimlazimu kiongozi huyo kusimama na kuzungumza nao.

Hata hivyo Magufuli amewaagiza mameneja wawili wa TANROADS Mkoa wa Lindi na Pwani kutotoa kazi kwa Kampuni hiyo hata kama ni ya kufagia hadi hapo itakapokamilisha ujenzi na kukabidhi barabara hiyo.

Awali Meneja wa TANROADS Pwani Tumaini Sarakikya amesema kampuni hiyo iliingia mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo km 57 na iliyokuwa Wizara ya Miundombinu Agosti 16 mwaka 2008 kwa gharama ya sh. Bilioni 58.8 na hadi sasa wameshakamilisha km 40 na kwamba km 17 ndiyo imebakia

Kwa upande wake mkandarasi wa kampuni hiyo ya M.A Kharafi and Sons,  Walid Mosalam na mshauri wake Wondwossen Dejene walipohojiwa sababu za kuchelewa kukamilisha mradi huo walijitetea kuwa inatokana na mafuriko ya mara kwa mara, kutopata fedha za ujenzi huo kwa wakati, uhaba wa vifaa hali ambayo huwalazimu kukodisha, ubovu wa mashine ya kuzalisha lami na utozwaji kodi katika vifaa vya ujenzi.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa