Home » » Chadema wazuiwa kujenga matawi ya chama Kibaha

Chadema wazuiwa kujenga matawi ya chama Kibaha

Chama cha Demokrasia na maendeleo Chadema kimelalamikia hatua ya viongozi wa halmashauri kuwazuia kujenga matawi ya chama hicho katika lengo zima la kutekeleza ilani ya chama chao.

Diwani wa Kata ya Tumbi, BW. MBENA MAKALA amesema hayo kufuatia vuta nikuvute kati yao na watu wanaodaiwa kutumwa na wakubwa kusitisha ujenzi wa tawi lao ikiwa sehemu ya utekelezaji wa kazi zao za siasa.

Bw. MAKALA amebainisha kuwa imekuwa vigumu kwao wanapotaka kujenga matawi ya chama chao kwa madai ya kuwa wanahitajika kuwa na vibali vinavyowaruhusu kujenga.

Ambapo BW.MAKALA amebainisha kuwa imekuwa tofauti na wenzao wa chama tawala ambao wamekuwa wakijenga mashina ya wakereketwa na matawi bila kusumbuliwa na vyombo vya dola, na kuichukulia hali hiyo kama ukandamizaji wa demokrasia nchini.

Diwani huyo alishangazwa na diwani wa CCM kata ya Mailimoja BW.ANDREW LUGANO  kujaribu kusimamisha ujenzi wa tawi hilo kwa madai ya kutekeleza maagizo kutoka kwa wakubwa.

Na wananchi walipotaka kujua ameagizwa na mkubwa gani hakumtaja, hata hivyo mwandishi wa habari hizi amefanikiwa kuongea na diwani huyo wa Kata ya Mailimoja kutaka kujua mtu aliyemuagiza kusimamisha ujenzi huo na kudai ni mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Kibaha.

Juhudi za kuwasiliana Mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Kibaha, BI.JENIFA OMOLO zilishindikana kwa sababu alikuwa kwenye kikao na mkuu wa wilaya ya Kibaha.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa