Home » » Aua mke mwenza kwa kumchoma kisu tumboni

Aua mke mwenza kwa kumchoma kisu tumboni

TATU Abdalah (37) mkazi wa Rufiji anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoani Pwani kwa tuhuma ya kumchoma kisu tumboni mwanamke Hajra Rashid na kumsababishia kifo kwa wivu wa kimapenzi baada ya kumtuhumu kuwa na mahusiano na baba watoto wake.

Inadaiwa kuwa chanzo cha Tatu kufanya mauaji hayo ni wivu wa kimapenzi ambapo marehemu anadaiwa alikuwa ana mahusiano ya kimapenzi na mume wa mtuhumiwa huyo Omar Abdalah ambaye hata hivyo hadi tukio hilo linatokea walishatalikiana mwaka mmoja uliopita.

Kaimu kamanda wa Polisi Mkoani Pwani,kamishna msaidizi Yusuph Ally amethibitisha tukio hilo ambapo amesema limetokea jioni juzi na kwamba mtuhumiwa alimvamia ghafla mwenzake nyumbani kwake na kumchoma kisu tumboni huku akimtuhumu kuwa na mahusiana na mume wake  aitwaye Omar .

Kamanda Ally amesema baada ya tukio hilo marehemu alikimbizwa kituo cha afya cha Muhoro na kabla hajapatiwa matibabu alifariki dunia.

Hata hivyo uchunguzi wa awali umebaini kuwa katika kipindi walichokaa Omar na Tatu kama mke na mume walibahatika kuzaa  watoto watano lakini kutokana na kutokuelewa mambo kadhaa mwaka mmoja uliopita walitalikiana na kila mtu kukaa kivyake.

Kaimu Kamanda huyo ameongeza kuwa baada ya muda huo Tatu alipata taarifa kuwa mtalaka wake alishajenga mahusiano ya kimapenzi na marehemu Hajra ambaye alikua jirani yake na kisha kumfuata marehemu huyo nyumbani kwake na kumchoma kisu .

Kamanda  Ally amebainisha kuwa mtuhumiwa huyo alipata urahisi wa kutenda tukio hilo  kutokana na kuishi eneo jirani  na tayari amekamatwa na polisi ili akajibu tuhuma inayomkabili.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa