Home » » Mawasiliano Msata-Bagamoyo yakatika, ni baada ya daraja kuvunjika

Mawasiliano Msata-Bagamoyo yakatika, ni baada ya daraja kuvunjika

MAWASILIANO baina ya wananchi wa Msata na wenzao wa Bagamoyo yamekatika kwa siku nne sasa baada ya daraja kubwa la muda linalounganisha barabara kuu ya Bagamoyo Msata kuvunikwa kabisa na maji yanayotokana na mvua zinazoendelea kunyesha na hivyo mamlaka husika mkoani Pwani kulazimika kuchukua hatu ya kuifunga barabara hiyo kwa muda hadi hapo maji hayo yatakapopungua.

Daraja hilo kubwa lililojaa maji ni lile linalounganisha barabara kuu ya lami ya Bagamoyo Msata njia ambayo ujenzi wake ulizinduliwa rasmi mwishoni mwa mwaka jana na Rais Jakaya Kiwete na matarajio ni kuanza kutumiwa mapema mwakani na magari yote ya mizigo na abiria wanaosafiri kwenda mikoa ya kaskazini na wanaotoka huko kuja Dar esalaam huku lengo kuu likiwa ni kupunguza foleni kubwa katika Barabara kuu ya Dar esalaam Morogoro.

Akizungumzia kufungwa kwa barabara hiyo huko eneo la tukio LEO, Meneja wakala wa barabara TANROADS Pwani,mhandisi Tumaini Sarakikya amesema baada ya kuona daraja hilo la muda limejaa maji wamelazimika kuifunga njia hiyo ili kuzuia maafa yanayoweza kutokea kwani kuna uwezekana mkubwa wa magari kusombwa na maji kwenye eneo hilo kutokana na maji hayo kuwa na nguvu.

Sarakikya amesema kwa kufungwa barabara hiyo kwa sasa wanashauri magari yote yasiyozidi tani kumi yanayotaka kusafiri kwenda mikoa ya kaskazini kutoka Dar esalaam watumie barabara mbili za Makofia Mlandizi kilomita 35 kutoka Bagamoyo ambapo watatokea Mlandizi mjini katika barabara ya Dar esalaam Morogoro na kuendelea na safari yao na ingine ni barabara ya Mapinga-Vikawe -Tamco kutokea bagamoyo ambapo nao watatokezea Kibaha mjini na kuendelea na safari zao.

Amesema tayari wameshaweka vibao vya matangazo kuelimisha Umma wasitumie tena wakati huu barabara hiyo ya Msata Bagamoyo na pia kutokana na kutambua uwepo wa wakorofi wanaong'oa alama za barabarani pia wameweka vifusi vya udongo kuzuia kabisa madereva wakaorofi wasiweze kupita hapo.

Naye Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Urlich Matei akiwa eneo la tukio amewataka wananchi kuacha tabia ya kulazimisha kuvuka eneo hilo la daraja kwani ni hatari maji ni mengi na yana nguvu yanaweza kuwasomba na kusabisha vifo na hivyo amewashauri kuzingatia agizo hilo hadi hapo maji yatakapopungua.

Hata hivyo kamanda Matei amesema siku ya kwanza na pili wamebaini kuwepo ukiukwaji wa agizo hilo ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakiondoa magogo na baadhi ya vizuizi vilivyowekwa kuzuia watu na magari wasipite hapo na sasa jeshi hilo litaimarisha ulinzi katika eneo hilo.

Barabara hiyo ya Msata Bagamoyo ina urefu wa kilomita 64 na ndiyo inayotarajiwa kuwa barabara kuu ya kupitisha mabasi na magari yote yatokayo na kwenda mikoa ya ukanda wa Kaskazini kutoka Dar esalaam na inajengwa na kampuni ya M/S Estim Contruction Company na kusimamiwa na M/S H.P Gauff Injeneure GMBH and Company kutoka nchini ujerumani kwa gharama ya sh. Bilioni 89.6 na hadi muda huu ujenzi wake umefikia asilimia 90.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa