JESHI la Polisi mkoani Pwani
limesema wamefanikiwa kupata vifaa vya kitaalamu vya kubaini vilevi na kwa sasa
wameanza kutumia vipimo hivyo maalumu vya ulevi kuwabaini madereva wanaoendesha
magari huku wakiwa wamelewa ama wametumia kilevi chochote kile wakati wakiwa
kazini na kuwachukulia hatua za kisheria.
Kamanda wa Polisi mkoani humo
Ulrich Matei amesema hayo kwenye kikao cha pamoja na wanahabari mkoani ambapo
aliongeza kuwa tayari vipimo 100 vya ulevi vimesambazwa katika wilaya zote na
lengo kuu ni kudhibitia ajali zinazotokea kwenye barabara kuu zinazotokana na
ulevi wa madereva.
Matei amesema awali jeshi hilo
lilikuwa na kipimo kimoja tu cha ulevi mkoa mzima hali ambayo ilikuwa ikiwawia
vigumu kudhibiti ajali zitokanazo na ulevi ambavyo vimekuwa vikitokea katika
maeneo kadhaa mkoani humo.
Aidha akizungumzia suala la
usalama, Kamanda Matei amesema wameimarisha ulinzi ambapo wameanzisha mitaa 51
ya kiusalama mkoani humo na inaongozwa na viongozi wa serikali za mitaa ambao
wanapaswa kuhakikisha wanatoa taarifa wakati wowote kwa viongozi wa jeshi hilo
wilayani pale tu inapotokea ama kuhisi uwepo wa matishio ya uhalifu au uvunjifu
wa amaani hivyo askari kuweza kuwahi eneo la tukio la kutatua tatizo husika.
Ameongeza kuwa tangu kuanzishwa
mitaa hiyo 51 ya kipolisi Mkoa huo hivi sasa ni shwari na kuahidi kuendelea
kutoa ushirikiano wa hali ya juu na wadau wa usalama ili kuliwezesha jeshi hilo
kutekeleza majukumu yake ipasavyo kwani bila jamii shirikishi hakuna usalama wa
kutosha.
0 comments:
Post a Comment