Home » » MAMA SALMA KIKWETE AWAANGUKIA WANAUME JUU YA UZAZI WA MPANGO

MAMA SALMA KIKWETE AWAANGUKIA WANAUME JUU YA UZAZI WA MPANGO

WANAUME nchini wametakiwa kuacha uoga,imani potofu na aibu bali wafahamu kuwa hata wao wana kila sababu ya kuhudhuria katika vituo vya kutolea huduma za afya ya uzazi ili na wao waweze kushiriki kikamilifu kwenye mchakato wa uzazi wa mpango nchini na siyo kuwaachia wake zao pekee ndiyo wawe wahudhuriaji wa huduma hizo vituoni huku na wao wakiwa ni wazazi.

Rai hiyo kwa wanaume imetolewa Aprili 22 na Mke wa Rais Jakaya Kikwete ,mama Salma Kikwete wakati akizindua wiki ya chanjo ya watoto Duniani ambapo kitaifa imefanyika kwenye viwanja vya shule ya Msingi Mtongani wilayani Kibaha mkoani Pwani.

Katika uzinduzi huo pamoja na mambo mengine kuhusu chanjo ya watoto chini ya mwaka mmoja,Mama Salma pia ametumia fursa hiyo kueleza kuwa akina baba wengi bado wanaonekana kuwa wazito kuungana na wake zao kwenda kujiunga na uzazi wa mpango ukilinganisha na idadi ya wanawake wanaojitokeza ambapo takwimu za sasa zionyesha kuwa kati ya wanaume mia moja ni mwanamme mmoja ama wawili tu ndiyo wanaoambatana na wake zao katika zoezi hilo.

Mama Salma alisema alisema takwimu hizo pia zimeonyesha wanaume hao wachache wanaofika vituoni wao hujiunga na uzazi wa mpango wa matumizi ya kondom na siyo njia zingine mbambali zilizopo ikiwemo za muda mfupi na mrefu na hivyo alishauri sasa ni vema kina baba na kima mama kwa pamoja wajenge utaratibu wa kuhudhuria vituo vya afya kupata huduma za uzazi wa mpango maana wao ni sehemu ya familia na ndiyo wana wajibu wa kuwalinda na kuwatunza viumbe wanaowatarajia kuwazaa.

Awali akimkaribisha mke huyo wa rais kuhutubia,Naibu Waziri wa afya na ustawi wa jamii,Seif Rashid amesema nchi ya Tanzania ni moja kati ya chi 6 zinazopunguza vifo vya watoto kwa kasi kubwa ambapo imefanikiwa kupunguza vifo hivyo kwa watoto walio chini ya miaka mitano kutoka  watoto 147 kwa mwaka 1999 hadi kufikia watoto  65 huku wa chini ya mwaka mmoja ni watoto 99 hadi 45 kwa kila vizazi 1000.na kwa watoto wachanga vifo pia vimepungua kutoka watoto wachanga 40 kwa mwaka 1999 hadi watoto 26 kwa kila vizazi 1000.

Naye Mwakilishi kutoka shirika la afya duniani ( WHO) Dkt  Faro Chatola amesema takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa chanjo huzuia takribani vifo milioni mbili hadi tatu kila mwaka kutokana na  maradhi yanayikingwa kwa chanjo duniani na hapa nchini Tanzania mafanikio yameonekena ya kutokomeza ugonjwa wa Ndui,donda koo,,Kifaduro,polio na pepopunda na ushahidi huo ameuona huko Ifakara katika hospiatlia ya St. francis ambapo wodi za surua na magonjwa hayo zimefungwa hakuna wagonjwa.

Mwakilishi huyo wa WHO amesisitiza mafanikio ya awali yaliyopataika kutokna na chanjo ya watoto yarejewe wakati huu wa wiki ya chanjo Duniani  kwa kuhakikisha watoto wote wasiopata chanjo kabisa wanafikiwa na pia kwa wale waliopata wanafatiliwa ili kuzikamilisha dozi yake utaratibu ambao utawezesha kutekelezwa lengo la nne la milenia hapa nchini.
mwisho.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa