Home » » MAENEO MATATU YANAYOONGOZA KWA MATUKIO YA UHALIFU KIBAHA YATAJWA

MAENEO MATATU YANAYOONGOZA KWA MATUKIO YA UHALIFU KIBAHA YATAJWA



Mwandishi wetu, Kibaha

MAENEO matatu ya Maili Moja, Picha ya ndege na Mlandizi yametajwa katika halmashauri ya mji wa Kibaha kuwa ndiyo yamekuwa yakiongoza kwa matukio ya uhalifu ambapo kwa kipindi cha hivi karibuni zaidi ya matukio 10 yametajwa kufanyika kwenye sehemu hizo.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na Usalama Wilayani Kibaha Halima Kihemba huko Mlandizi wakati akizungumza na watendaji, madiwani na wananchi ambao walikuwa wamehudhuria kwenye kikao cha Baraza la Madiwani.

Kihemba ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo amesema hali ya uhalifu umeanza kushamiri katika halmashauri hiyo huku akitaja maeneo hayo ya Maili Moja, Picha ya Ndege na Mlandizi kuwa ndiyo sehemu zilizokithiri kwa matukio ya uvunjifu wa amani.

Kutokana na hali hiyo,Kihemba amewataka viongozi wote wakiwemo wa siasa wakashirikiane na wananchi kwenye maeneo yao kuwabaini wahusika wa matukio ya uhalifu ili sheria iweze kuchukua mkondo wake kwa lengo la kukomesha hali hiyo.
  
Amesema pia wananchi wana nafasi ya kujua walipo vijana wao hasa nyakati za jioni kwani wapo baadhi ya vijana wadogo nao wamekuwa wakirubuniwa na kisha kujiingiza kwenye matukio hayo huku mzazi nyumbani akiwa hajui lolote.

Mkuu huyo wa wilaya ameshauri wazazi watumie muda mwingi kukaa na vijana wao wakiwaelimisha watoto wao kutojiingiza katika makundi yasiyo salama hasa ya uvutaji bangi ambayo ndiyo wengi wao huwalaghai wenzao hao kujiingiza katika uhalifu.

Mkoani Pwani Wilaya tatu za Kibaha, Bagamoyo na Rufiji ndiyo halmashauri pekee zilizotajwa hivi karibuni kuongoza kwa matukio ya uhalifu ikilinganishwa na zingine za Mafia, Kisarawe na Mkuranga.
mwisho

Blogzamikoa

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa