Na Gustaphu Haule, Kibaha
WAKAZI wa Wilaya ya Kibaha Vijijini mkoani
Pwani, wametakiwa kuacha tabia ya kuwaozesha watoto wao wa kike wakiwa na umri
mdogo na badala yake wawaendeleze kielimu ili iweze kuwasaidia katika maisha
yao ya baadaye.
Wito huo ulitolewa jana na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Janeth Sylvanus, katika mahafali ya
Shule ya Sekondari Kilangalanga, iliyopo Mlandizi, Kibaha Pwani.
Sylvanus alisema tabia ya kuwaozesha watoto wa kike wakiwa na umri mdogo ni
vitendo vya ukatili ambavyo kwa sasa vinapigwa vita kila siku, hivyo akawataka
wazazi wenye tabia hiyo kuacha mara moja tabia hiyo, ili kuwapa fursa watoto
hao kuendelea na masomo yao.
Alisema ili kukomesha vitendo hivyo ni vyema Serikali ikaweka mpango madhubuti
ambao utawabana wazazi wenye tabia hizo kwa kuwakamata na kuwapeleka katika
vyombo vya sheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.
“Ndugu zangu elimu ni msingi wa maendeleo kwa kila Mtanzania hivyo ni vizuri
kama wazazi wakawa na mwamko wa kuwasomesha watoto wao ili wapate hazina ya
baadae lakini vitendo vya kuwaozesha watoto mapema ni kukiuka na kuwanyima haki
zao za msingi ,” alisema.
Sylvanus alisema yupo tayari kushirikiana na wazazi pamoja na bodi ya shule
hiyo ili kuhakikisha wanaweka misingi sawia itakayowasaidia wanafunzi wa shule
hiyo kusoma kwa bidii na kupata elimu bora zaidi.
Katika mahafali hayo, kada huyo aliahidi kuwasomesha wanafunzi 50 wa shule hiyo
wanaoishi katika mazingira magumu pamoja na kuwalipia ada wanafunzi 12 wa
kidato cha nne watakaofaulu kujiunga na kidato cha tano, mwakani.
Shule ya Sekondari Kilangalanga ilianzishwa mwaka 1995 ikiwa na wanafunzi 80,
lakini mpaka sasa inajumla ya wanafunzi 1,499, wakiwamo wavulana 744 na wasichana
755 ambapo hata hivyo wanafunzi wa kidato cha nne wanaohitimu mwaka huu ni 209
wasichana 109 na wavulana 100.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment