Home » » MAHIZA AWAANGUKIA WAISLAMU KUSHIRIKI SENSA

MAHIZA AWAANGUKIA WAISLAMU KUSHIRIKI SENSA

na Julieth Mkireri na Victor Masangu, Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza amewaomba waumini wa dini ya Kiislamu kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa na kuachana na upotoshwaji unaofanywa na baadhi ya viongozi wao ambao wanawapa vitisho.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Mahiza aliwaomba viongozi wa dini hiyo kama watakuwa na hoja zao, watumie utaratibu kuzifikisha sehemu husika ili zifanyiwe kazi kabla ya siku ya sensa, Agosti 26 mwaka huu.
Alisema kuwa baadhi ya viongozi wa dini ya Kiislamu wamekuwa wakitoa vitisho kwa waumini wa dini hiyo kutoshiriki katika zoezi hilo kwa madai ambayo hawajayafikisha sehemu husika ili waweze kupatiwa ufumbuzi.
“Mimi mwenyewe ni Muislamu, lakini nawasisitiza waumini wenzangu kutoa ushirikiano kufanikisha zoezi hili ambalo litasaidia kufanikisha adhma ya maendeleo yetu, kwani kila mtu atapata fursa ya kueleza kile anachojihusisha nacho na itatuwezesha pia kupanga namna ya kuwasaidia wananchi watu baada ya kujua maisha yao halisi,” alisema Mahiza.
Mahiza aliwaomba viongozi hao kutafuta namna ya kuwasilisha hoja zao kwa kuweka madai yao vizuri na kuyawasilisha sehemu husika, ili yaweze kufanyiwa kazi na kufanikisha kufanyika kwa zoezi hilo ambalo ni wajibu wao kushiriki.
Katika hatua nyingine Mahiza alitoa wito kwa wakulima wa korosho kuwa na subira juu ya suala lao la kutafutiwa soko la kuuzia zao hilo badala ya kutishia kutoshiriki katika zoezi la sensa.
Wakulima hao wa korosho wanadaiwa kutaka kugoma kutokana na korosho zao zaidi ya tani 8,000 kuendelea kudoda katika ghala lililopo Mbagala Zakhiem jijini Dar es Salaam kwa takribani miezi nane sasa, huku msimu wa pili ukikaribia kuanza.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa