Home » » JKT RUVU YAPIGWA TAFU VIFAA

JKT RUVU YAPIGWA TAFU VIFAA


na Clescencia Tryphone
TIMU ya soka ya JKT Ruvu inayoshiriki Ligi Kuu Bara, imekabidhiwa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya sh milioni 6 na benki ya CRDB.
Vifaa hivyo ni pamoja na nguo za mazoezi na kusafiria, jezi pamoja na mipira kwa ajili ya ligi hiyo itakayoanza Septemba 1.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo, Mkuu wa Idara ya Uendeshaji CRDB, Samson Keenya alisema, wameamua kutoa vifaa hivyo, ikiwa ni sehemu ya mchango wao katika jamii na kuwa, wataendelea kuwapa sapoti zaidi ya hapo.
“Tumeamua kutoa vifaa hivi kwa timu hii na sisi tutaendelea kuwasapoti zaidi na zaidi na kutokana na sapoti yetu kwa timu hii, tutahakikisha inafanya vema katika Ligi Kuu Tanzania Bara,” alisema Keenya.
Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Samwel Ndomba, ambaye alipokea vifaa hivyo, aliishukuru benki hiyo kwa kuwasapoti na kuwa, kilichobaki ni changamoto kwa Kocha na wachezaji ili waweze kufanya vema katika ligi hiyo.
“Tunawashukuru sana CRDB, ila sasa ni kazi kwetu kuonyesha matunda mazuri, ikiwa ni kushika nafasi ya kwanza na ya pili itwaliwe na JKT Oljoro na wengine wafuate na pia nawaomba wadhamini siku nyingine mdhamini mambo mbalimbali ndani ya JKT na sio soka pekee,” alisema Meja Jenerali Ndomba.
Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa Ruvu JKT, Charles Killinda, aliwapongeza wadhamini hao na kuwa, waendelee na moyo huo huo wa kuziangalia timu za chini na sio kila siku Simba na Yanga, wakati zina wadhamini wengi.
“Nawashukuru sana na nina ahidi kuwafurahisha sana na nimejipanga zaidi ligi msimu ujao, kwa kuwa nina kikosi bora maana nafasi ya Rajabu Chau aliyevunjika mguu tayari imezibwa na Musa Hassan Mgosi, nina imani kikosi changu kitafanya vema zaidi ya msimu uliopita,” alisema Killinda.
Aliongeza kuwa, mara baada ya kumalizika kwa michuano ya Sita bora Agosti 25 wanatarajia kucheza mchezo wa kujipima na mabingwa wa soka Afrika Mashariki na Kati, Yanga.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa