Home » » DC MAFIA AZINDUA UVUNAJI WA JONGOO

DC MAFIA AZINDUA UVUNAJI WA JONGOO

Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Mhe. Aziza Mangosongo amezindua uvunaji wa jongoo bahari katika kitalu kilichopo kijiji cha Dongo, kitongoji cha Mfuruni Julai 30, 2024.

Uvunaji huo wa jongoo bahari umezinduliwa rasmi kwa mara ya kwanza ambapo Mhe. Mangosongo amempongeza mfugaji wa jongoo bahari, mzee Mpogo kwa mchango wake wa kendeleza uchumi wa buluu pamoja na kuleta fursa ya ajira kwa vijana.

" Tumevutiwa sana, vijana wengi wangepatiwa elimu na kujishughulisha na ufugaji wa jongoo bahari, basi wangejikwamua na tatizo la ajira. Kwa upande mwengine, mradi huu unatunza mazingira na ndivyo ambavyo viongozi wetu, hasa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anavyotutaka kujikita katika uchumi wa buluu na kutunza mazingira" alisema Mhe. Mangosongo.

Kwa upande wake, Mfugaji wa jongoo bahari Mzee Waziri Mpogo, ameipongeza Serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Halmashauri kwa kutoa ushirikiano kuwezesha fursa hiyo kuwepo pamoja na kuwaomba wakazi wa Mafia wajitokeze kufanya shughuli hiyo ili kuifungua wilaya zaidi kwenye suala la uchumi wa buluu.

Lengo langu ni kutaka wafugaji wadogo wadogo waweze kupata mbegu hapahapa Wilayani badala ya kuzifuata Bagamoyo ama sehemu nyingine" alisema Mzee Mpogo. Nimepata faraja pia kuona mazingira yapo salama kwa sababu mradi huu unasaidia kutunza mazingira, hivyo nawaomba viongozi na wananchi wote tushirikiane katika kukuza uchumi wa buluu" aliongeza.

Mradi huo uliogharimu Shilingi Milioni 176, umekuwa msaada kwa vijana kwa kuwasaidia kuwapa fursa ya ajira.

" Nawaomba vijana wenzangu kujitokeza katika mradi huu badala ya kujishughulisha na mambo ya uhalifu, tunaweza pia kuunda kikundi chetu na kujikwamua kiuchumi" alisema Salum Alawi, kijana anayefanya kazi katika kampuni ya Mpogo Ocean Ranching inayojihusisha na ufugaji wa jongoo bahari.

 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa