Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MKE
wa rais mstaafu ,mama Salma Kikwete ,akiwa katika maadhimisho ya siku
ya mtoto wa kike kimkoa Mkoani Pwani yaliyofanyika Kibaha na kufadhiliwa
na shirika lisilo la kiserikali la Room To Read linalotekeleza mradi wa
kumwendeleza mtoto wa kike.Picha na Mwamvua Mwinyi
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
MKE
wa rais mstaafu ,mama Salma Kikwete,amesema mkoa wa Pwani upambane na
mafataki wanaoteka fikra za watoto wao wa kike ili kuondokana na mimba
za utotoni ambapo mkoa huo ni kati ya mikoa kumi inayoongoza kwa mimba
hizo kitaifa.
Aidha
amekemea tabia inayofanywa na mashuga dadi wanaojiona mahodari wa
kutongoza na kunyemelea watoto wa kike wanafunzi na wengine kuwakatisha
masomo kwa kuwatia mimba na kudai anaejiona hodari wa kutongoza dunia
aende kwa wanawake wakubwa huko mitaani.
Pamoja
na hilo,Mama Salma ,ameitaka jamii kuachana na mila na desturi
zinazochochea mimba ,na kusema lazima zitazamwe ili kuwawezesha watoto
hao waendelee na masomo yao.
Aliyasema
hayo,wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike
kimkoa,yaliyofanyika wilayani Kibaha mkoani Pwani,ambayo yamefadhiliwa
na shirika lisilo la kiserikali la Room To Read.
Alisema
mkoa unaoongoza kwa mimba za utotoni ni mkoa wa Katavi wenye asilimia
45 ambapo mkoa wa Pwani upo ndani ya mikoa kumi inayoongoza kwa mimba
hizo ukiwa na asilimia 30.
Mama
Salma alisema,mimba za utotoni hazikubaliki ,watoto wa kike wajitambue ,
na wajijue wao ni lulu ,na thamani ya mtoto wa kike ni kufunga
mapaja,wafunge mapaja yao na wakifunga mapaja hakuna mdudu atakaeingia.“Situmii
kitu kinachoitwa tafsida hapa,naongea kama ilivyo ili mzidi kunielewa
na walengwa yawaingie kikamilifu kichwani mwao”,alisema mama Salma.
Alisema ni wakati wa mkoa huo kuongoza kielimu na kuwa kumi bora kitaaluma badala ya kuongoza kwenye mimba za utotoni.Hata
hivyo Mama Salma alieleza kwamba,tabia inayofanywa na baadhi ya wazazi
wanaodiriki kufanya mapenzi na watoto wao wa kike ni lazima ilaaniwe
duniani kote,ili kukomesha vitendo hivyo vya aibu.
Alisema
dunia ya leo imeharibika kwani wapo wazazi ambao wanawabaka ama
kuwafanya mapenzi watoto waliowazaa wenyewe bila ya kuona aya.Alieleza
pia,vijana na wazee(mashuga dadi) wanaokimbilia watoto wadogo waliopo
mashuleni waache tamaa za kimwili na atakaebainika atafungwa miaka 30
jela .
Mama
Salma aliitaka jamii kuheshimu na kujali watoto wa kike maana ni nguzo
ya maendeleo ya taifa ,dhana potofu zikomeshwe zinazowanyanyapaa na
kuwadhalilisha watoto wa kike na ikumbukwe malezi na makuzi ya watoto wa
kike ni wajibu kwa kila mmoja kwenye jamii .“Unavyoona
huwezi kufanya mapenzi na mtoto wako basi usijaribu kufanya mapenzi na
mtoto wa jirani yako,kwani mtoto wa mwenzio ni wako,”
Mama
Salma aliwaambia wazazi na walezi, watenge muda wa kuwafundisha
kujikinga na majaribu wanayokutana nayo kwenye mzunguko wa maisha
yao,wawape haki za msingi zinazostahili ikiwa ni sanjali na elimu sawa
na watoto wa kiume.Aliwaasa
na wanafunzi wa kike wakubaliane na hali ya maisha waliyonayo wazazi
wao wasiwe na tamaa hali inayosababisha kupata vishawishi.
Mama
Salma,aliwahusia watoto hao watumie stadi walizopatiwa kama silaha ya
kujikinga na maadui hivyo wasikubali kuzima ndoto zao na elimu .
“Someni
msikimbilie kuolewa ,mtapata mnachokitaka hadi mtachoka,wanaume wapo
tuu,serikali inahimiza msome na kuwawekea misingi mizuri ya kielemu
ikiwemo kusomeshwa bure, acheni mchezo,jilindeni”
“Ni
haki ya mtoto wa kike nae kujilinda,ajitunze ili siku moja afikie ndoto
zake kuwa mwalimu,mainjinia ama madaktari bingwa.mawaziri, makamu wa
rais”.Mama
Salma alielezea,kwasasa nchi inajivunia kuwa na naibu katibu mkuu wa
kwanza mwanamke wa umoja wa mataifa kutoka Tanzania,Asharose Migiro
,makamu wa rais mwanamke wa kwanza Samia Suluhu Hassan na waziri wa
fedha wa kwanza Tanzania Zakia Meghji.
“Wapo
wengi nikiwataja hapa hawatoshi ,hawa wametupa heshima na wamefika hapo
kutoka na elimu,jaribuni kufanya bidii mfikie malengo yenu,“Ninawausia
ni lazima kuienzi elimu kwanza,tunahitaji walimu kutoka nchini sio nje
ya nchi,na kuacha kubeza ualimu kuwa kwenda ualimu ni hadi ukose kazi
nzuri nyingine ,alifafanua Mama Salma.
Katika
hatua nyingine alisema anaimani kutatiliwa mkazo kwa kuingiza somo la
stadi za maisha katika mtaala wa shule nchini ili kujenga wasichana
waweze kujisimamia na kujitambua wenyewe .Mama
Salma alisema,tumekuwa tukijifunza mengi kupitia miradi mbalimbali ya
kufundisha stadi za maisha ikiwemo kupambana na mimba za utotoni.
Alitoa
wito kwa wadau wa elimu ,halmashauri kuchangia changamoto hizo kwa
kutenga bajeti za ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wa kike katika shule za
sekondari”,Sanjali na madarasa na maabara kwani itakuwa rahisi
kuzungumza na mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali yaweze kusaidia
kirahisi.
Nae
mkuu wa wilaya ya Kibaha,Assumpter Mshama ambae alimwakilisha mkuu wa
mkoa huo,alisema zipo baadhi ya mila na desturi zipo mkoani hapo ambazo
zinachangiua kukatisha masomo ya watoto kwa kuwaoza kabla ya kumaliza
masomo yao.
Alisema
utoro na mimba mkoani Pwani ni sababu kubwa inayoshusha taaluma kwa
watoto kijumla kwani kwa mwaka huu watoto wa kike 61 wa darasa la saba
mkoani hapo wamepata mimba na kushindwa kufanya mitihani yao ya mwisho.Assumpter
alieleza ,utoro ni 58 ,vifo sita na magonjwa ni 12 hivyo watoto
watambue umuhi wa kujiendelea kielimu kama ufunguo wao wa maisha.
Kwa
upande wake,afisa elimu mkoa wa Pwani ,Germana Sondoka alisema
wataendelea kusimamia maelekezo ya serikali na kimataifa ambayo
yanahusika kumlinda mtoto wa kike ili aweze kutimzia ndoto zake.
Alisema
watahakikisha wanafunzi mkoani humo hasa wa kike wanafikia malengo yao
na kutokomeza vitendo vinavyochangia kumkatisha mtoto huyo masomo yake.
Germana
alieleza kufuatia kaulimbiu ya kutokomeza mimba za utotoni kufikia
uchumi wa viwanda ,watashirikiana baina ya serikali mkoa,maafisa
elimu,walimu na wanafunzi kwa kuendelea kuitafsiri kauli hiyo kwa
vitendo.
Mkurugenzi
wa shirika lisilo la kiserikali la Room To Read,wanatekeleza mradi wa
kumwendeleza mtoto wa kike ,Peter Mwamanga,alisema shirika hilo lilianza
mwaka 2012 ambapo wanafundisha pia stadi za maisha kwa wanafunzi wa
shule za msingi na sekondari.
Alisema
mtoto wa kike amekuwa akipambana na changamoto nyingi hadi kufanikiwa
na kujikuta zipo anazokutana nazo na kusababisha ndoto zake zikififia
siku hadi siku.Mwamanga
alitoa wito kwa wadau mbalimbali kushirikiana kutokomeza vitendo vya
mimba za utotoni na kupambana na wale wanaokatisha masomo ya watoto hao.
Room
To Read walichukua fursa hiyo kumpatia tuzo mama Salma ya kutambua na
kuthamini mchango wake wa kuwakomboa na kupambana kutetea haki za mtoto
wa kike na mimba za utotoni,kupitia WAMA.
0 comments:
Post a Comment