Home » » AZAM WAZIKARIBISHA SIMBA NA YANGA AZAM COMPLEX

AZAM WAZIKARIBISHA SIMBA NA YANGA AZAM COMPLEX

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.  

Afisa habari  wa Azam Fc Jaffar Iddy.

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.

UONGOZI wa Klabu ya Azam umefurahiswa na maamuzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF) kwa kuamua kutumia Uwanja wa Azam Complex kwa michezo ya nyumbani ya timu hiyo.

Hilo limekuja baada ya Bodi ya Ligi kutoa ratiba mpya na kuzitaka timu za Simba na Yanga kwenda kucheza mechi zao dhidi ya Azam katika Uwanja huo.

Akizungumza kwa niaba ya klabu ya Azam, Afisa habari Jaffar Iddy ameupongeza uongozi huo chini ya Rais mpya wa TFF Wallace Karia kwa kusimamia haki kwa kila timu kucheza katika uwanja wao wa nyumbani.

Iddy amesema kuwa, kwa miaka kadhaa wamekuwa wakilalamika hasa kushindwa kuutumia uwanja wao wa nyumbani na kwenda kutumia Uwanja wa Taifa kama wenyeji pindi wanapocheza na timu za Yanga na Simba.

"tumefurahishw ana maamuzi ya TFF na bodi ya ligi chini ya Rais Wallace Karia kwa kuamua klabu za Simba na Yanga kuja kucheza katika Uwanja wetu wa Azam Complex kwani miaka mingi sana hasa katika uongozi uliopita ulishindwa kufanya maamuzi hayo na kutunyima haki yetu ya msingi,"amesema Iddy.

Iddy amesema anawakaribisha sana Simba na Yanga katika Uwanja wa Azam kwani anakumbuka timu hizo zilishwahi kucheza kwenye Uwanja huo kipindi ambacho uwanja wa Uhuru ukiwa umefungwa.

Akiongelea maandalizi kuelekea mchezo wao Jumamosi dhidi ya Simba, Iddy amesema kuwa timu yao imejipanga vizuri kwa mchezo huo na kikosi kipo kambini wakiendelea kujifua zaidi ila watawakosa wachezaji wao wawili ambao wote ni majeruhi wakiwa katika matibabu.

Amewataja wachezaji hao ni Shaban Iddy Chilunda na Joseph Kimwaga aliyoko nchini Afrika Kusini akisubiri matibabu na akitarajiwa kufanyiwa upasuaji siku ya Alhamis.

Azam itavaana na Simba katika mchezo wa pili wa ligi kuu Vodacom huku baadhi ya wachezaji wa zamani wa timu wakiwa wamejiunga na Simba wakicheza kwa mara ya kwanza toka kuondoka katika klabu hiyo.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa