Imeandikwa na John Gagarini, Bagamoyo
WATU watatu wakiwamo watoto wadogo wawili wamekufa huku wawili
wakinusurika baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kuzama kwenye mto
Ruvu, walipokuwa wakijaribu kuvuka kutoka Vigwaza kwenda Mlandizi mkoani
Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi wa Mkoa,
Jonathan Shana alisema licha ya watu hao kubainika kufa, nahodha wa
mtumbwi huo hajulikani alipo. Shana alisema ajali hiyo imetokea Jumamosi
saa 4:00 asubuhi kwenye mto Ruvu wilaya ya kipolisi Chalinze.
“Ajali hiyo imepoteza maisha ya watoto wawili ambao ni Nusrat Haji
miezi minne na Feisal Hamza mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu pamoja na
Sikuzani Musa (41), ambaye mwili wake bado haujapatikana,” alisema
Kamanda Shana.
Kamanda Shana aliwataja walionusurika ni Zuwena Ramadhan (29) na Tero
Mziray (20) ambapo dereva wa mtumbwi huo hajulikani alipo na inaaminika
hakufa maji. “Chanzo cha mtumbwi huo kuzama bado kinachunguzwa na miili
ya marehemu imefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa ndugu zao kwa ajili ya
mazishi,” aliongeza. Aliwataka wamiliki wa vyombo hivyo kuhakikisha
vinakuwa kwenye hali nzuri ili kuepukana na ajali kama hizo ambazo
zinapoteza uhai wa watu kutokana na ubovu.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment