Imeandikwa na John Gagarini, Bagamoyo
HUKU serikali ikiwa inaweka mikakati ya kukabiliana na wimbi la
wahamiaji haramu nchini, Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limewakamata
wahamiaji haramu 72 kutoka Ethiopia kwa tuhuma za kuingia nchini bila ya
kibali.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Kituo cha Wilaya ya
Kipolisi Chalinze, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Jonathan Shana alisema
wahamiaji hao walikuwa safarini kwenda Afrika ya Kusini.
Kamanda Shana alisema wahamiaji hao walikamatwa Jumamosi saa 3:30
asubuhi kwenye Pori la Ranchi ya Taifa (NARCO) Kata ya Vigwaza, Chalinze
wilayani Bagamoyo. “Mbali ya wahamiaji hao haramu, pia tunamshikilia
Rajabu Hitaji (30) mkazi na mfanyabiashara wa Vigwaza baada ya msako
mkali uliofanywa na makachero wa Jeshi la Polisi baada ya kupata taarifa
kuwa kuna wahamiaji haramu wameingia bila ya kibali,” alisema Kamanda
Shana.
Alisema wahamiaji hao haramu baada ya kugundua kuwa kuna gari la
polisi linawafuatilia, waliingia kwenye hifadhi hiyo kwa lengo la
kujificha, lakini msako mkali uliofanywa uliwabaini na kukamata kundi la
kwanza la watu 63 ambao walikaa sehemu ambayo gari haliwezi kufika.
“Baada ya kuwakamata wahamiaji hao haramu kundi la kwanza askari
waliendelea na msako ambapo waliwakamata wahamiaji wengine tisa
waliokuwa wakijaribu kutaka kutoka kwenye pori hilo,” aliongeza Kamanda
Shana. Alisema wahamiaji hao haramu wanatarajiwa kukabidhiwa Idara ya
Uhamiaji kwa ajili ya hatua za kisheria pamoja na mfanyabiashara
aliyekamatwa anayetuhumiwa kuwasafirisha.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment