John Gagarini, Kibaha
KUTOKANA na kukithiri kwa ajali za mabasi madogo aina ya Noah,
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) mkoani
Pwani imesitisha utoaji leseni mpya kwa magari hayo yanayojulikana zaidi
kwa jina mchomoko na Hiace katika barabara kuu zote, ikiwamo ya
Morogoro.
Noah pamoja na pikipiki zimeelezwa kusababisha vifo vya watu 102 huku
246 wakijeruhiwa katika kipindi cha kuanzia 2015 hadi Machi 2016.
Akizungumza na wanahabari mjini Kibaha, Ofisa Mfawidhi wa Sumatra
mkoa wa Pwani, Nashon Iroga, alisema kwa mujibu wa waraka walioupata
kutoka makao makuu, magari hayo yote madogo ya abiria yanayokwenda
masafa marefu kupitia barabara kuu hayatapewa leseni ya kubeba abiria.
“Barabara kuu kuna vyombo vikubwa vya usafiri hivyo hayataruhusiwa
kupata leseni mpya, badala yake yaliyokwisha pata leseni yataendelea
hadi hapo mwongozo mwingine utakapo tolewa,” alisema Iroga.
Alisema, agizo hilo limetolewa baada ya ongezeko kubwa la magari
madogo ya kubeba abiria hasa magari aina ya Noah, kufanya safari ndefu
huku baadhi yakiwa yamebeba abiria na mizigo bila kuangalia usalama wa
abiria na matokeo yake ni kusababisha ajali za mara kwa mara na
msongamano katika barabara kuu.
“Ukiangalia kwa hali ya kawaida magari aina ya Noah yanabeba abiria
wachache lakini ili wapate faida inabidi watoze viwango vikubwa vya
nauli, kubeba abiria kuliko uwezo wake na kwenda mwendo kasi ili wafanye
safari nyingi na kupata faida, matokeo yake wanahatarisha usalama wa
maisha ya abiria,” alisema Iroga.
Aidha, alisema magari hayo madogo yakiwamo Noah na Hiace yanayobeba
abiria yatapewa lesseni mpya za kufanya biashara kutumia ruti za
barabara za ndani na sio barabara kuu.

0 comments:
Post a Comment