Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji
wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha kuziandikia barua taasisi mbalimbali
zilizochukua viwanja kwenye kitovu cha Mji kwa nini zisinyang’anywe kwa
kushindwa kuviendeleza kwa muda mrefu.
Aliyasema hayo mjini Kibaha alipokuwa akizungumza na watendaji wa
halmashauri hiyo na kusema kuwa taasisi hizo zimekiuka taratibu za
uendelezaji ardhi ambazo huwataka kuendeleza eneo kwa kipindi cha miezi
36.
Ndikilo alisema licha ya taasisi hizo kuandikiwa barua na ofisi yake
zikitakiwa kuviendeleza viwanja hivyo mwaka 2015, lakini zilikaidi agizo
hilo hivyo kuona kuwa kuna haja ya kuzinyang’anya na kuzipa taasisi
nyingine ambazo ziko tayari kujenga kwa wakati.
“Tumeshapitia Kibaha kupanda hadhi na kuwa Manispaa na tunasubiri
taratibu mbalimbali ili kukamilika azma hiyo ndiyo maana tulizipatia
taasisi hizo eneo lake maalumu kwa ajili ya kujenga ofisi ambazo
zingeonesha mandhari nzuri ya mji, lakini walengwa wameshindwa
kutekeleza taratibu za uendelezaji,” alisema Ndikilo.
Alisema sheria inaeleza kuwa kama mtu kashindwa kuendeleza eneo kwa
kipindi cha miezi 36, halmashauri ina uwezo wa kumnyang’anya na kumpa
mwingine ili aendeleze eneo husika, hivyo taasisi hizo zimeshavunja
utaratibu.
“Tulitarajia wangejenga majengo ya kisasa ili kuwa kivutio na kwa
kuwa inakuwa Manispaa lazima majengo yake yawe mazuri,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa nakala za barua hizo zipitie ofisini kwake na kwa Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kuzifutia hati
taasisi zilizoshindwa kuendeleza viwanja hivyo ambavyo viko katikati ya
mji huo.
CHANZO : HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment