Home » » TASAF YANUSURU KAYA MASKINI 5,600 KIBAHA.

TASAF YANUSURU KAYA MASKINI 5,600 KIBAHA.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) wilayani Kibaha mkoani Pwani, umetoa Sh milioni 216.2 kupitia mpango wa kunusuru kaya masikini wilayani humo kwa kipindi cha miezi miwili.
Hayo yalisemwa kwenye kijiji cha Magindu na Mratibu wa Mpango huo, Godson Harry wakati wa ugawaji wa fedha za uhawalishaji kwa kaya masikini awamu ya tatu kwenye kijiji hicho, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, alikuwa mgeni rasmi.
Harry alisema fedha hizo zimetolewa kwa walengwa 5,600 hadi Februari mwaka huu, kwa ajili ya huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na afya pamoja na elimu kwa kaya hizo.
“Fedha hizo ambazo ni ruzuku zinazotolewa ni za aina mbili ikiwa ni pamoja na ruzuku ya msingi inayozihusu kaya masikini kwa lengo la kuondoa umasikini kwa kufanya kazi ili wajipatie ujira kupitia kazi za mikono,” alisema Harry.
Alisema kuwa ruzuku ya pili ni ruzuku ya masharti ambayo inahusu kaya masikini zenye watoto wanaosoma au wanaohudhuria kliniki na lazima watimize masharti hayo ikiwa ni pamoja na kuhudhuria shuleni pamoja na kliniki kwa wakati ili zipewe ruzuku hiyo.
Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi, Issa Seleman, alisema kijiji hicho kina kaya 410 zinazonufaika na mpango huo na tayari kimepokea awamu 12 kwa walengwa na awamu hii kinapokea Sh milioni 12.8.
Seleman alisema mafanikio walioyapata ni kuanzisha vikundi 21 kwa sasa na hali ya umasikini imepungua ikiwa ni pamoja na magonjwa kwani walengwa wamehudhuria zahanati kwa asilimia 95 ikilinganishwa na kabla ya mpango huo ilikuwa asilimia 55, huku changamoto ikiwa ni pamoja na walengwa 26 kudai Sh 897,000 na kiwango kinachotolewa kuwa kidogo.
Kwa upande wake, Ndikilo alisema kuwa ili fedha hizo ziweze kuwa na mafanikio lazima walengwa wawe na nidhamu ya matumizi ya fedha hizo ili malengo ya serikali yaweze kufikiwa.
 CHANZO ; HABARI LEO.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa