Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid.
Ugawaji wa vitambulisho hivyo ulizinduliwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Jeniffer Omolo, mjini hapa jana.
Hatua hiyo inafuatia siku chache baada ya serikali kutoa agizo kwa
halmashauri zote nchini kuwatambua wazee wastaafu hususan wenye umri wa
kuanzia miaka 60 na kuendelea na kuwapa vitambulisho vitakavyowafanya
watibiwe bure ikiwa ni njia sahihi ya kutambua juhudi zao za kulitumikia
taifa wakiwa na nguvu.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Dk. Issessanda Kaniki,
alisema uorodheshaji wa wazee wote kwa kupita nyumba kwa nyumba
ulifanyika kwa kusaidiana na Kitengo cha Ustawi wa Jamii na Good
Samaritan ‘Help Age’ International ambapo jumla ya wazee 4,672
waliandikishwa.
Aidha, Dk. Kaniki aliongeza kuwa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi
ya mwaka 2012, inaonyesha kuwa Halmashauri ya Mji Kibaha ina wazee
5,111.
"Hivyo baada uzinduzi huu wa leo (jana), ofisi yangu itapita tena
kwenye mitaa yote 73 kuwahamisisha wazee ambao hawakupiga picha za
vitambulisho wapige ili wapate vitambulisho vya matibabu bure," alisema.
Aidha, Omolo aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, aliwataka
watumishi wa Idara ya Afya kuzingatia maadili ya kazi yao na kuwahudumia
wazee hao kikamilifu.
Pia aliwataka kuandaa madirisha maalum kwa ajili yao na kwamba
hatarajii kusikia manung’uniko na malalamiko kutoka kwa wazee hao.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi na Huduma za Jamii Mheshimiwa
Tuaje Ponza, aliwataka wazee nchini kutambua juhudi za Serikali kuwajali
na kuwa wao ni watu muhimu kwani maendeleo yaliyopo leo wameyachangia
kwa kiasi kikubwa na wao.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wazee wenzake, Eleuter Kigodi,
alisema wamefarijika mno kuona serikali inatambua utumishi na uzalendo
wao kwa nchi yao na kuahidi kuunga mkono juhudi zozote za serikali.
Halmashauri ya Mji wa Kibaha kwa kutumia fedha ya mapato yake ya
ndani, ilitenga Sh. 11,650,000.00 zilizotumika kutengeneza vitambulisho
4,672 kwa ajili ya wazee.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment