SERIKALI imeyata
Mabaraza ya wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya juu kote nchini kufanya kazi kwa
bidii na kuzingatia weledi, kanuni na sheria zinazosimamia mabaraza hayo ili yawe chachu katika kuleta
maendeleo ya Elimu na mabadiliko ya
kiuchumi ya taasisi hizo.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Fedha (Sera) Mhe. Mwigulu
Nchemba wakati akizindua Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Taasisi ya Uhasibu
Tanzania (TIA) lililojumuisha wawakilishi kutoka matawi 6 ya taasisi hiyo katika mikoa ya Kigoma, Singida, Mwanza ,
Mtwara, Dar es salaam na Mbeya.
Mhe. Mwigulu amesema kuwa
iwapo mabaraza hayo yatazingatia weledi katika kusimamia masuala mbalimbali ya
taasisi hizo nchini yataleta mabadiliko
ya kiutendaji katika usimamizi wa mapato na matumizi na kutoa
ushauri utakaoisaidia Serikali kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo.
Mhe. Mwigulu
ameeleza kuwa endapo mabaraza hayo yataacha
kufanya kazi kwa mazoea na kujikita katika kuzingatia kanuni na taratibu
zilizowekwa, taasisi hizo zitaongeza uzalishaji, zitakuza mapato na kutatua
kero mbalimbali za wafanyakazi mahali pa kazi.
“ Napenda niweke wazi
kuwa mabaraza haya ni muhimu sana kwa
wafanyakazi, hayana tofauti na bunge ,kazi yake
kubwa ni kusimamia mapato na matumizi, kushauri taasisi na Serikali juu
ya utekelezaji wa mipango mbalimbali
ikiwemo ajira kwa watumishi wapya” Amesisitiza.
Akizungumzia changamato
ya uhaba wa walimu na watumishi wa kada mbalimbali katika taasisi hiyo na taasisi nyingine za
Umma za Elimu ya juu amesema Serikali inaendelea kutenga fedha katika bajeti ya kila mwaka ili
kuondoa tatizo hilo.
Aidha, amesema Serikali
inaendelea kulishughulikia suala la usimamizi wa ziada ya mapato yanayozalishwa
na taasisi za umma ili yaweze kupelekwa
katika maeneo mengine yenye uhitaji.
“Serikali tunaendelea
kuangalia utaratibu wa kutumia ziada ya mapato inayozalishwa na taasisi
mbalimbali za umma ili iweze kupelekwa katika maeneo mengine yenye uhitaji
maana fedha hizi ni za umma,taasisi moja ya Serikali haiwezi kung’ania ziada ya
mapato iliyozalisha, hizo ni fedha za umma lazima zikafanye kazi maeneo mengine
yenye uhitaji hasa kwenye kugharamia mahitaji ya wodi za akina mama kote
nchini”
Pia amesisitiza mkakati
wa Serikali wa kuzifanya taasisi hizo za elimu ya juu kuwa na mamlaka yake
katika kuajili watumishi wake na kjitegemea.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye ndiye Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania Dkt.
Joseph Kihanda akizungumza na wajumbe wa
baraza hilo amesema kuwa taasisi hiyo katika kipindi cha miaka 5 imepata
mafanikio makubwa ya kuongeza ukusanyaji
wa mapato kutoka shilingi Bilioni 6 za mwaka 2010 hadi kufikia shilingi Bilioni
18 mwaka 2014/2015.
Amesema Taasisi hiyo
licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya uhaba wa miundombinu,
ufinyu wa bajeti , uhaba wa walimu wenye shahada za uzamivu (PhD) na watumishi kimeendelea kupata idadi kubwa ya
wanafunzi wanaodahiliwa kutoka 7635
waliodahiliwa mwaka 2011/2012 hadi kufikia 14974 mwaka 2014/2015.
“Licha ya kuendelea
kufanya vizuri taasisi yetu inakabiliwa na tatizo la waalimu katika matawi yetu
yaliyo mikoani ,jambo hili hutufanya tutumie gharama kubwa kuwasafirisha kutoka
makao makuu kwenda kufundisha wanafunzi wetu wanaochukua michepuo ya Biashara,
Uhasibu, Rasilimali Watu, Ununuzi na Ugavi,Uhasibu katika Sekta ya Umma na
Masoko na Mahusiano kwenye matawi yetu” Amesisitiza.
Naye Mwenyekiti wa Bodi
ya ushauri ya wizara ya Fedha wa Taasisi hiyo Prof. Isaya Jairo akizungumza na
wajumbe waliohudhuria mkutano huo amesema kuwa Taasisi ya Uhasibu Tanzania
(TIA)katika kukuza na kuongeza mapato ya ndani na kupunguza utegemezi kutoka
serikalini itaendelea kufanya shughuli kibiashara ,kufanya utafiti, kutoa ushauri
katika Nyanja za uhasibu, ununuzi na ugavi kote nchini.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment