Niwe mkweli; nilichukia sana kwa wezi na matapeli kupachikwa
a.k.a. ya “wasanii”. Niliona wazi jinsi mbunifu mwenye uwezo wa
kutafsiri ujumbe unaotoka kwenye ubongo hata ukasomeka na watu wa rika
zote, anavyopewa hadhi sawa na mjinga asiyejua kutafuta riziki kwa njia
halali. Ni tusi kubwa lisilomithilika kwa lugha yoyote duniani, hata
akhera!
Lakini hivi majuzi nilianza kufikiria iwapo chuki
yangu ilikuwa na tija. Ilikuwa ni baada ya “msanii” (huyu acha nimwite
hivyo kwa kweli) kuja kitaani kwangu kabisa, akacheza muvi ya ukweli ya
nusu saa na kuondoka. Kila shuhuda alishangazwa na baadhi walijikuta
wakishangilia baada ya kuielewa picha ile. Jamaa alicheza sini nne za
muvi halisi ambayo bila shaka baadaye inaweza kuigizwa.
Picha lilianza jamaa akiwasili na taxi
iliyojulikana baadaye kuwa ilikodiwa Buguruni. Lokesheni ilikuwa
nyumbani kwa mjumbe wa shina wa chama tawala, akajitambulisha kuwa ni
ndugu wa mkazi wa kitongojini hapo aliyefariki dunia ghafla. Hivyo,
baada ya kupata taarifa, amekuja ili kumpumzisha nduguye kwenye nyumba
yake ya milele.
Baada ya kutoa pole, mjumbe alimwelekeza jamaa
njia za kufuata; aende Serikali ya Mtaa kupata barua ya uthibitisho
Kiserikali, na kanisani au msikitini kwa huduma za kiroho kwa marehemu.
Jamaa alijibu kuwa alilitambua hilo, na pale alipo yupo kamili. Alidai
kuwa hatua yake ya kwanza katika muda huo ilikuwa ni kuwasiliana na
wachimba kaburi na kununua chakula cha waombolezaji.
Mjumbe hakuwa na hiyana, alipiga simu na kufumba
na kufumbua wachimbaji walikuwa pale. Jamaa yetu akaomba “profoma
invoisi” ya kaburi la kujengwa kwa tofali na kupigwa plasta. Wajenzi
walikuwa tayari kuelewana bei badala ya kuambizana kwa viingereza; mara
“foma” mara “voisi wanda”.
Jamaa akafungua mlango wa taxi na kupekua kati ya
mafaili yake. Alipokosa alichokihitaji alichomoa simu lake la kupangusa
na kulichomoa laini. “Nani ana simu yenye chaji?” Wachimbaji walitoa
simu zao, akachagua moja yenye kiwango na kutia laini yake. Akawaagiza
wachimbaji wengine watangulie kuchimba kaburi. “Ingia kwenye gari
tukatoe fedha kwa wakala,” alimuagiza yule mwenye simu.
Jirani na wakala jamaa aliona bucha. Alimuagiza
dereva apaki mbele ya bucha. Aliingia pale na kuagiza nyama ya kutosha
kwa shughuli ya msiba. Alimuagiza muuza nyama aikatekate kabisa wakati
yeye akipata huduma kwa wakala maana alikuwa nyuma ya wakati. Mambo
yalitakiwa kwenda fasta sana.
Akavuka upande wa pili kwa wakala: “Naweza kutoa
fedha ya kutosha kwenye mtandao wa (kampuni moja ya simu)?” Wakala
aliitikia kukubali. Jamaa akabofya “*xxx*xxx#”, lakini ghafla alikunja
uso na kujishika chini ya kibofu. “Mnayo huduma ya choo hapa?” Wakala
alimwelekeza kilipo choo na kuendelea kuhudumia wateja wengine.
Nusu saa ikapita. Dereva alimfuata wakala
kumuuliza ‘wapi bosi?’ Akajibiwa kuwa tangu alipokwenda msalani hakupata
kujua nini kilimsibu huko. Alikwenda kumtazama kurudi na swali: “Kwani
hauna namba yake ya simu?” Kwa ujumla, iliwachukua zaidi ya saa mbili
kutambua kuwa walidanganywa! Haidhuru, walikwenda kuzika mgomba kaburini
na maisha yakaendelea kama mwanzo.
Kitu kilichonifanya nimkubali huyu kuwa msanii ni
stahimili yake. Alihitaji simu tu, lakini aliwahusisha dereva wa taxi
kutoka Buguruni, mjumbe wa nyumba kumi, wachimba kaburi, muuza nyama na
wakala. Ukifikiri kwa undani unaweza kudhani kuwa akili za yule mwizi wa
simu zilikuwa na kichaa.
Uchaa gani wakati alifanikiwa katika azma yake? Hata kama lengo halikuwa jema mbele za wengi, lakini alifanikiwa.
Msanii anaruhusiwa kuongopa ili lengo lake
(kuelimisha) lifanikiwe. Yupo aliyemwimbia mpenzi wake “Sema utakacho...
hata ndege nitanunua” wakati yeye binafsi hata baiskeli ilimshinda.
Naamini hata yule aliyeimba “Sitarudia tena. Nikirudia tena ning’oe
meno...” hakulisema hilo kwa dhati. Laiti angelimwona siku moja mpenzi
akimjia na koleo, basi pangechimbika kwelikweli.
Si kwamba namsifia huyu mwizi asiye na haya wala huruma, kwa
kutokwa na udenda na kusumbua umati wa watu kwa kitu kidogo sana. Bali
mnyonge tumnyonge lakini haki yake tumpe. Ni muhimu huyu mtaalamu asakwe
na kukamatwa. Lakini badala ya kutunukiwa kifungo jela, apewe adhabu ya
kuufunza umma namna ya kumtambua na kumkwepa mtu wa aina yake.
Kila wakati una changamoto zake. Tulishuhudia wakati ukipita na vifungo vya wavumbuzi wa magobole yaliyotumia risasi za nondo.
Tulishuhudia pia yule bingwa wa mawasiliano wa
uswahilini akiukimbia mji wake kutokana na msako mkali wa Jeshi la
Polisi dhidi yake. Huyu mtaalamu alizalisha chaneli ya redio
iliyozisumbua idhaa za redio za Serikali.
Zama hizi tusimhukumu mwalimu kwa suti zake. Tujali chakula cha ubongo kwa faida ya kizazi chetu na kijacho.
Na sisi tumtumie tapeli wetu hasa katika kipindi
hiki cha Uchaguzi Mkuu. Wanaotaka uongozi kwa udanganyifu watakuja na
mbinu mpya na za kale. Wanaotajwa kuwa wezi wa kura watakuja na mbinu
kama hizo. Tunataka atuelekeze namna ya kuwatambua watu wanaofanana
naye.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment