MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imetakiwa kutoa elimu kwa
wafanyabiashara hasa inapotokea mabadiliko katika mfumo wa ulipaji kodi
ili kuepusha migogoro ya mara kwa mara kati ya mamlaka hiyo na walipa
kodi.
Wito huo umetolewa mwishoni mwa wiki na Katibu Tawala Wilaya ya
Mkuranga mkoani Pwani, Epifania Mosha, wakati akizungumza na
wafanyabiashara na watumishi wa mamlaka hiyo wakati wa kilele cha wiki
ya mlipa kodi.
Mosha, alisema ukosefu wa elimu kwa wafanyabishara kuhusiana na
mabadiliko ya mfumo wa ulipaji kodi, ni moja ya chanzo cha migogoro
inayosababisha wafanyabiashara kugoma huku mamlaka nayo ikisimama
kukusanya kodi kutoka kwa wateja wao.
Kwa upande wake, Meneja wa mamlaka hiyo mkoani Pwani, Highness
Chacky, alisema elimu ya kodi imekuwa haipewi kipaumbele na
wafanyabishara kutokana na muamko mdogo pale wanapotakiwa kushiriki.
Chacky, pia alisema hadi sasa mashine za kieletroniki za EFD
hazitumiki kama inavyotakiwa, kutokana na wafanyabiashara wengi
kuendelea kutoa risiti ambazo zimeandikwa kwa mkono.
Aliwapongeza watumishi wa mamlaka hiyo mkoani hapa kwa kazi
wanayoifanya, ambako wamefanikisha kukusanya zaidi ya sh bilioni 6
Julai hadi Oktoba na kuvuka malengo ambayo ilikuwa sh bilioni 5.69.
Aliwataka wafanyabiashara kuwa na ushirikiano na TRA, ili kama kuna
changamoto waweze kuzitatua kwa pamoja badala ya kukimbilia kufunga
biashara zao.
Chanzo;Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment