Home » » HALMASHAURI KIBAHA KUCHANJA MBWA 5,000

HALMASHAURI KIBAHA KUCHANJA MBWA 5,000

HALMASHAURI ya Mji Kibaha mkoani Pwani imeanza kutoa chanjo ya kichaa cha mbwa ili kuwanusuru wananchi na ugonjwa hatari wa kichaa cha mbwa.
Chanjo hiyo muhimu inafanyika katika kata 14 na mitaa yote 73 ya halmashauri hiyo na inatarajiwa mbwa zaidi ya 5000, watachanjwa kwa wiki moja. Chanjo ilianza jana.
Chanjo hiyo itawahusu wanyama wengine wanaowekwa kwenye kundi la wanyama wanaoweza kuwa na maambukizi ya kichaa cha mbwa, kama paka na mbwa mwitu, ambapo zaidi ya paka 200 watachanjwa kwenye mji huo.
Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Charles Marwa alisema Kibaha ni miongoni wa Halmashauri 24 zilizopo kwenye mradi wa kutokomeza ugonjwa wa kichaa cha mbwa, unaofadhiliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), taasisi ya Bill and Melinda Gates Foundation na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Marwa alisema wizara ya afya huwajibika kutoa chanjo kwa watu wanaong’atwa na mbwa au paka na kufanya tafiti mbalimbali zinazohusu ugonjwa wa kichaa cha mbwa.
Alisema Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni kuhakikisha wanyama wote wanaoweza kusababisha ugonjwa wa kichaa cha mbwa wanachanjwa ili kutokomeza maradhi ya kichaa cha mbwa nchini.
Mratibu wa mpango wa kuchanja mbwa wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Ramadhani Mohamed alieleza kuwa kichaa cha mbwa ni ugonjwa hatari unaosababishwa na virusi jamii ya rhabdoviridae na huwapata wanyama na binadamu wanapong’atwa na mnyama mwenye virusi vya ugonjwa huo kama vile mbwa, mbwa mwitu, paka na fisi.
Chanjo hiyo itagharimu zaidi ya Sh milioni 14. Huu ni mwaka wa nne mfululizo kwa Halmashauri ya Mji Kibaha kuchanja mbwa na paka. Mwaka 2013 chanjo hiyo ilifanikiwa kwa asilimia 85.

Chanzo:Habari Leo
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa