Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MADIWANI wa Halmashauri ya Mji Kibaha, wamemshukia Mweka Hazina wa Halmashauri hiyo kutokana na kusuasua kwa malipo ya wakandarasi na watu wengine huku kukiwa hakuna sababu maalumu.
Wakizungumza kwa jazba katika kikao cha Baraza la Madiwani mjini hapa, walisema hawako tayari kuendelea kumvumilia mtumishi anayezorotesha utoaji huduma kwa wananchi na kuifanya Halmashauri kutupiwa lawama.
Diwani wa Kata ya Mailimoja, Andrew Lugano, alisema wapo baadhi ya wakandarasi wamelalamikia kucheleweshewa malipo ya kazi zao ambazo wamefanya, huku wakishindwa kupewa sababu za msingi kutoka kwa Mweka Hazina huyo.
“Watu wanafanya kazi halafu hawalipwi fedha zao kwa wakati na huyu Mweka Hazina hatoi sababu za kuchelewesha hayo malipo… ana kazi ya kuwapiga kalenda watu wazima, wanakuja kila siku na kurudi bila mafanikio, hii sio haki hata kidogo inaleta sifa mbaya kwa Halmashauri yetu,” alisema Lugano.
Aidha, kutokana na madiwani walio wengi kutaka Mweka Hazina huyo awajibishwe baada ya kuwepo kwa tuhuma nyingi zinazomkabili za kuchelewesha malipo bila sababu, diwani wa viti maalumu, Selina Wilson, aliomba itolewe nafasi ili asikilizwe atoe sababu endapo zina mashiko apewe muda kujirekebisha.
“Naomba waheshimiwa madiwani wenzangu, kabla ya kufanya lolote tumpe nafasi ili aeleze sababu zilizokuwa zinamkwamisha kutoa malipo kwa wakati, inawezekana Mkurugenzi akawa ndio chanzo, tumsikilize tutoe maamuzi,” alisema Wilson.
Kabla ya kutoa muda kwa Mweka hazina kusikilizwa, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Adhudad Mkomambo, aliungana na madiwani wengine kutoa taarifa za malalamiko kutoka kwa watu mbalimbali waliofanya kazi katika Halmashauri hiyo na malipo yao kuendelea kusuasua hadi sasa.
Mweka hazina huyo, Suzana Chaula, alipopewa muda wa kujieleza, alisema hawezi kukataa kama idara yake ina mapungufu huku yeye akiwa kama msimamizi, isipokuwa tuhuma hizo si zake kwa kuwa yeye si muandaaji wa malipo.
“Kwanza niseme kwamba mimi sina mtu wa kunikingia kifua ngazi za juu ni mtumishi kama walivyo wengine na nikikosa nastahili kuwajibishwa kama walivyo watumishi wengine, kwa malalamiko haya naomba radhi mimi mwenyewe kwa kutosimamia vizuri watumishi wa idara yangu,” alisema Chaula.
Baada ya maelezo hayo, Diwani wa Picha ya Ndege, Bosco Mfundo, aliomba utolewe muda kwa mweka hazina huyo kujirekebisha kutokana na utetezi wake na itakaposhindikana hatua zichukuliwe.
Tuhuma zilizoelekezwa kwa mweka hazina huyo ni pamoja na kuchelewesha malipo kwa wakandarasi waliofanya kazi za Halmashauri hiyo na malipo kwa wakufunzi wa TASAF.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment