Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MCHAKATO wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kumpata mgombea uenyekiti wa Kijiji cha Kihangaiko Tarafa ya Msata wilayani Bagamoyo, Pwani, mwishoni mwa wiki umeingia dosari baada ya wajumbe kunusurika kuzichapa hadharani wakati kila kundi likitaka mgombea wake apite.
Mzozo huo uliibuka baada ya msimamizi wa uchaguzi huo, Adamu Kitegire, akiungwa mkono na Wana-CCM kutoka tawi la Madesa, kutangaza kuahirisha mkutano huo na kuzichoma moto kura zilizokuwa zimepigwa kuwachagua wajumbe wa serikali ya mtaa kwa madai kuwa, wanachama waliopiga hawakuwa halali.
“Naahirisha mkutano huu wa mchakato kupata wagombea hadi hapo itakapopangwa tena, sababu kubwa ni kuwa kwanza wengi wenu hapa sio wanachama halali wa CCM, hivyo hatuwezi kuendelea,” alisema Kitegire.
Kutokana na kauli hiyo, Mwenyekiti wa CCM tawi la Kihangaiko, Mohamedi Kisulu, akiungwa mkono na wanachama wake, alikataa na kumtuhumu msimamizi huyo kuwa anakusudia kuweka viongozi wake kwa maslahi binafsi badala ya wanaopendekezwa na wananchi.
Hata hivyo, baada ya tafrani hiyo iliyodumu kwa takribani nusu saa, Mwenyekiti Kisulu alizira kikao na kuondoka akiwaacha wajumbe wa mkutano huo wakiwa wamechachamaa wakishutumiana kwa maneno makali yakiwemo ya ubaguzi wa uzawa na kushikana mashati.
Kumeguka kwa wana CCM hao, kulikwenda mbali zaidi baada ya wanachama kutoka Madesa, kutamka wazi wazi kuwa kama mgombea wao hatapita basi watakiua chama kwa kumchagua kiongozi kutoka upinzani na hata kama atashinda mgombea wa chama hicho, hawatashirikiana naye hadi atakapoondoka madarakani.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment