Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi
Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango Bibi Florence Mwanri (aliyesimama) akimkaribisha
mgeni rasmi Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Pwani Bibi Mwantumu Mahiza (aliyekaa kaikati).
Kulia ni Katibu wa Baraza hilo Bw. Senya Robert.
Mgeni Rasmi wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Rais,
Tume ya Mipango, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Mwantumu Mahiza (aliyesimama)
akisisitiza jambo alipokua akifungua kikao cha Baraza hilo.
Wajumbe wa Baraza wakifuatilia kwa
makini majadiliano yaliyokua yakiendelea wakati wa baraza hilo.
Wajumbe wa Baraza la wafanyakazi
Ofisi ya Rais, Tume ya Mipando kwa pamoja wakiimba wimbo wa Solidarity Forever kuonyesha mshikamano
makazini.
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi,
Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango wakionyesha mshikamano kwa kuimba wimbo wa Solidarity forever mara baada ya Mkuu wa
Mkoa wa Pwani kufungua rasmi kikao hicho.
Picha ya pamoja
Kabla ya kuanza majadiliano,
wajumbe walimchagua Mwenyekiti Msaidizi wa Baraza la Wafanyakazi ambapo Bibi
Magreth Simwela (aliyesimama) aliibuka mshindi kati ya wajumbe watatu waliokua
wakigombea nafasi hiyo. Hapo Mwenyekiti Msaidizi alikua akiwashukuru wajumbe
kwa kumchagua.
======== -====== ========
MKUTANO WA BARAZA LA WAFANYAKAZI WA OFISI YA RAIS, TUME
YA MIPANGO KATIKA UKUMBI WA HOTELI YA JD COMPLEX – KIBAHA, PWANI.
HOTUBA YA MKUU
WA MKOA WA PWANI MH. MWANTUMU BAKARI MAHIZA KATIKA UFUNGUZI WA MKUTANO WA
BARAZA LA WAFANYAKAZI WA OFISI YA RAIS, TUME YA MIPANGO KATIKA UKUMBI WA HOTELI
YA JD COMPLEX – KIBAHA, PWANI.
·
Ndugu
Mwenyekiti
·
Mwakilishi
wa TUGHE Taifa
·
Mwakilishi
TUGHE Mkoa wa Dar es salaam
·
Mwenyekiti
wa TUGHE ORTM
·
Ndugu
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi
·
Mabibi
na Mabwana
Awali
ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kuwepo hapa leo hii
tukiwa na afya njema. Pia, nikushukuru
wewe binafsi Kaimu Katibu Mtendaji, pamoja na timu yako kwa kunipa heshima hii
kubwa ya kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya
Rais, Tume ya Mipango.
Ndugu washiriki,
Nimearifiwa
kuwa Baraza hili ni la kwanza katika mwaka 2014/15 na limewakilishwa na Wakuu
wote wa Klasta, Idara na Vitengo, wajumbe wa TUGHE Taifa, TUGHE Mkoa – Dar es
salaam, Halmashauri ya Tawi la TUGHE Tume ya Mipango na mjumbe mmoja mmoja
kutoka kila Klasta, Idara na Vitengo.
Aidha,
napenda kutumia fursa hii kuwapongeza wajumbe wote wa mkutano huu kwa
kuchaguliwa kwenu kuwa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Rais, Tume
ya Mipango kupitia mabadiliko ya Mkataba Mpya. Hii ni kutokana na imani kubwa
waliyonayo watumishi juu yenu katika kuwawakilisha katika chombo hiki
muhimu.
Ndugu washiriki,
Baraza
la Wafanyakazi ni kama Bunge la Taasisi yenu kwa kuwa linaundwa na wawakilishi
wa wafanyakazi wote waliochaguliwa kidemokrasia. Baraza hili ni chombo muhimu sana
kilichoundwa kisheria kwa madhumuni ya kuwashirikisha watumishi katika kujadili
na kufanya maamuzi kuhusu masuala yanayohusu maslahi ya ajira mahali pa kazi
kwa lengo la kuleta tija. Kupitia Baraza hili mwajiri anapokea maoni ya
watumishi na kuweza kufikia maamuzi sahihi ya namna ya kuboresha mazingira ya
kazi na watumishi kwa ujumla.
Wajibu
wa mabaraza haya kama vyombo vya ushauri na usimamizi ni kuhakikisha kuwa
waajiri na watumishi wanatambua wajibu na haki zao na wanazingatia maadili ya
utumishi wao ili kuleta matokeo makubwa ya utendaji kazi yenye tija.
Ndugu washiriki,
Hata
kama kutakuwa na sera, sheria na kanuni nzuri katika mahali pa kazi pasipokuwa
na ushirikiano baina ya mwajiri na watumishi itakuwa vigumu Taasisi kutimiza malengo yake. Hivyo pamoja na mambo mengine Baraza hili
lina wajibu wa kuishauri Tume kwa lengo la kuleta tija na mshikamano baina ya
mtumishi na mwajiri. Sio vizuri kwa watumishi kutumia muda mwingi katika kudai
maslahi zaidi kuliko kupima kiwango cha utekelezaji wa wajibu wao.
Moja
ya kazi za Baraza ni kuhakikisha kuwa watumishi wanatekeleza wajibu wao kwanza
kabla ya kudai maslahi na wanapodai maslahi wanatakiwa kufuata misingi ya
sheria na taratibu zilizopo.
Ndugu washiriki,
Tume
ya Mipango iliundwa chini ya Ofisi ya Rais kutekeleza majukumu ya msingi ambayo
ni kutoa dira ya maendeleo na mwongozo wa uchumi wa taifa, kubuni na kuishauri
Serikali kuhusu sera za menejimenti ya uchumi na mikakati ya maendeleo na kufanya
utafiti.
Ndugu Mwenyekiti na washiriki;
Napenda
kutumia nafasi hii kukupongeza Mwenyekiti kwa kushirikiana na wasaidizi wako na
watumishi wote kwa ujumla kwa kuweza kutekeleza majukumu mliyopewa kitaifa kwa
ufanisi. Nimeelezwa kuwa pamoja na changamoto
za uhaba wa rasilimali katika mwaka wa fedha 2013/14 mmeweza kutekeleza jukumu
kubwa la kutayarisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa, 2014/15 ambao uliwasilishwa
katika kikao cha Bunge cha mwezi Juni 2014, pamoja na majukumu mengine ambayo
ni kufuatilia utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2013/14 na kufanya
mapitio ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 –
2015/16), kusambaza machapisho mbalimbali ya Tume ya Mipango na kuandaa
Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma (Public Investment Management Manual).
Ndugu Mwenyekiti na washiriki;
Ni
matarajio yangu kuwa kwa kuzingatia taratibu na miongozo ya Serikali, Tume ya
Mipango mmepanga malengo mbalimbali ya kutekeleza katika mwaka wa 2013/14
ambapo hatimaye mtakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuishauri Serikali katika
masuala mbalimbali ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Kwa kusema hivi natumaini
kuwa michango yenu katika mkutano huu wa siku mbili, itatoa matokeo makubwa
yatakayoliwezeshaTaifa letu kusonga mbele kiuchumi.
Ndugu Mwenyekiti na washiriki;
Hivyo,
ni matumaini yangu kuwa kwa kutumia kikao hiki kama wajumbe wa Baraza la
Wafanyakazi mnayo nafasi kubwa ya kuwaelimisha wafanyakazi wenzenu kuhusu
umuhimu wa kila mmoja kutimiza wajibu wake katika sehemu yake ya kazi ili kufikia
malengo mliojiwekea. Njia pekee ya kufikia malengo yetu ni kila mmoja kufanya
kazi kwa bidii na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili kulitendea haki
Taifa letu. Kila mmoja wetu akemee kwa sauti watumishi wasiotimiza wajibu wao.
Wakuu wa Klasta, Idara na Vitengo wasimamie kwa dhati suala la maadili katika
sehemu zao za kazi. Tukumbuke kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
huelekeza kuwa kila mtu apate ujira unaolingana na wajibu aliotimiza.
Ndugu Mwenyekiti na washiriki;
Nimeelezwa
kwamba miongoni mwa mada zitakazowasilishwa na kujadiliwa katika mkutano huu ni
mafanikio ya utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka 2013/14 na kujadili taarifa ya
fedha za mwaka, elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, umuhimu wa mawasiliano
serikalini na uelewa juu ya kiwango kinachopaswa kutozwa kodi ya mapato
yatokanayo na ajira (mshahara).
Ndugu Mwenyekiti na washiriki;
Mwisho
napenda kutoa shukrani kwa kuwa Mgeni Rasmi katika mkutano huu muhimu na
kuwatakia majadiliano mazuri na yenye lengo la kuimarisha uhusiano mzuri kwenye
Taasisi yenu. Nihitimishe kwa kuwatakia
kikao chenye mafanikio yaliyokusudiwa.
Baada
ya kusema hayo machache, napenda kutamka kwamba ‘Mkutano wa Baraza la
Wafanyakazi la Tume ya Mipango Umefunguliwa Rasmi’!
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment