Home » » KIBAHA KUKUSANYA KODI KWA MAX MALIPO

KIBAHA KUKUSANYA KODI KWA MAX MALIPO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

 

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Mji Kibaha mkoani Pwani, Jenifa Omolo amesema halmashauri hiyo inatarajia kuanza kukusanya mapato yote ikiwemo kodi ya majengo kwa mfumo kama Max Malipo, hivyo kazi kubwa waliyonayo kwa sasa ni kuhakikisha wanapata takwimu sahihi za nyumba katika mitaa yao.

Hayo aliyasema katika mkutano wake na wenyeviti na watendaji wa serikali za mitaa pamoja na watendaji ikiwa ni utaratibu wake aliojiwekea wa kuwajengea uwezo wa namna ya kukusanya kodi ya majengo kwa wananchi wanaowaongoza.

Omolo aliwaambia kuwa Mji wa Kibaha unakua kwa kasi sana na kuwataka wanapotafuta takwimu za nyumba wajumuishe hata nyumba za udongo kwa kuwa maisha bora yanaongezeka siku hadi siku na wananchi nao wanakwenda sanjari na falsafa hiyo.

Aidha, alitoa angalizo kuwa iwapo hawatafanya hivyo upatikanaji wa takwimu sahihi hautafanikiwa.

Sanjari na hilo Omolo aliwataka watendaji kuwapa wananchi hati ya malipo (Demand Note) mapema kama namna ya kuwakumbusha kulipa kodi na kuhakikisha risiti zinatunzwa vema ili kuepuka usumbufu wa faini kwa atakayechelewesha malipo ama wa kumdai mwananchi mara mbili.

Omolo alitoa rai kwa wananchi wote wenye ardhi inayomilikiwa kisheria kulipia kodi mapema tena bila shuruti kwani kutokana na utaratibu wa kulipia kwa mfumo unaoanza anayekaidi anajikomoa mwenyewe kwa kujilimbikizia deni ambalo mwisho wa siku litagundulika.

"Mfumo huu ni mzuri kweli kweli, wale wanaotumia ujanja ujanja wa kutolipa kodi, mfumo utawatambua tu, ndivyo dunia inavyokwenda kwa sasa, hutakwepa sana sana utatozwa faini ya asilimia kumi ambayo ipo kisheria utakapogundulika," alisema.

Kwa upande wake mweka hazina wa Halmashauri Suzana Chaula aliwataka watendaji kuwasambazia wananchi hati za malipo (Demand note) na kutosahihisha chochote kilichomo kwenye hati hiyo kwani kwa kufanya hivyo wanaweza kuharibu utaratibu, hivyo masahihisho yote yatafanywa na wataalam wa mfumo.

Katika mkutano huo, Omolo alitumia fursa hiyo kuwakaribisha watendaji wapya walioajiriwa mapema mwezi huu kuziba nafasi za waliostaafu na kuwataka wafanye kazi kwa weledi na kuzingatia kanuni, taratibu na sheria za utumishi huku akiwasisitiza kuwa pamoja na jukumu kuu la kuwahudumia wananchi, pia watapimika kwa uwezo wao wa kukusanya mapato na kodi nyingine watakazoelekezwa.

Aliwataka kuishi kwenye vituo vyao vya kazi na kuacha visingizio vya kukosa nyumba huku akiwakumbusha kuwa kukaa nje ya mkoa wake kikazi ni kinyume cha sheria na iwapo kuna ulazima kwa kukaa huko ni kwa kibali maalum kutoka kwa mwajiri. Zaidi ya wenyeviti na Watendaji 120 walihudhuria kikao hicho.

Kodi ya majengo pekee imekadiriwa kukusanya zaidi ya sh. milioni 158 mwaka wa fedha 2014/15.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa