Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WAFANYABIASHARA
zaidi ya 50 wa mji wa Kibaha Mkoani Pwani, wamefunga maduka yao
kuwaunga mkono wafanyabiashara saba waliofungiwa maduka na Mamlaka ya
Mapato (TRA), mkoani hapa kutokana na kukosa mashine za EFD.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya wafanyabiashara mkoa wa Pwani, Abdallah
Ndauka alisema kuwa Septemba 9 mwaka huu maduka saba ya wafanyabiashara
wa mailimoja yalifungiwa, hali iliyosababisha wenzao kuungana nao
kutokana na kukosa mashine hizo.
Ndauka, alisema alishangazwa na kitendo cha TRA kufunga maduka hayo
huku wakishindwa kukutana na wafanyabiashara hao kujadiliana kuhusiana
na matumizi ya mashine hizo.
“Tunataka mabadiliko ya kimfumo, tunahitaji mashine zitambue gharama
za manunuzi na uendeshaji kitakachobakia kilipie kodi TRA, lakini pia
TRA wanatakiwa kutambua kuwa bidhaa nyingine hazina risiti,” alisema.
Aidha Ndauka alisema, malalamiko yao kwa kushirikiana na Jumuiya ya
wafanyabiashara ngazi ya taifa yalishafika kwa Naibu Waziri wa fedha
Mwigulu Nchemba ambaye aliahidi kuyafanyia kazi,baada ya kuombwa
kukutana na TRA kushughulikia suala hilo.
Naye Mohamed Lutambi, alisema hatua ya kufunga maduka hayo
imewaathiri na kuwakandamiza kwa kuwa wanategemea biashara hizo kwa
ajili ya kupata fedha za kuendesha maisha yao.
Akizungumzia malalamiko hayo Ofisa Elimu na Huduma kwa Mlipa Kodi wa
Mamlaka hiyo, Bakari Kapera, alisema wafanyabiashara waliofungiwa maduka
kila mmoja ana kosa lake sio suala la mashine pekee.
Kapera, alisisitiza kuwa mashine za EFD ni sawa na vitabu vya risiti
na inatunza kumbukumbu sahihi kwa kila bidhaa inayouzwa, ambapo
aliwashauri wafanyabiashara hao kushiriki kwenye mikutano inayoitishwa
na mamlaka hiyo badala ya kutuma wawakilishi.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment