Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MBUNGE wa Kisarawe, Seleman Jafo, amewasihi wakazi wa jimbo hilo
kuzingatia uchangiaji wa mfuko wa maji ili kuwezesha miradi
inayotekelezwa kuwa endelevu na kuondokana na kero ambayo imekuwa
ikiwakabili kipindi kirefu.
Jafo, alitoa wito huo wakati akizungumza na wananchi wa vijiji vya
Kihale, Panga la Mwingereza na Chole, baada ya kukagua maendeleo ya
ujenzi wa miradi ya maji inayotekelezwa katika jimbo hilo.
Alisema kuwa atashangaa kuona kuna mwananchi anashindwa kuchangia
asilimia 2.5 inayotakiwa kuchangiwa na wanakijijiji kwenye mfuko wa
maji, kwani fedha hizo ndizo zitakazowasaidia kukarabati miundombinu
pale inapotokea imechakaa ama kuharibika.
Mbunge huyo alisema kuwa, kamati za maji zinatakiwa kusimamia
kikamilifu uchangiaji wa fedha hizo, kwani serikali haitaweza kumudu
kugharamia vitu vingine baada ya mradi kukamilika na hivyo mchango wa
wananchi ndio utakaowezesha miradi hiyo kudumu kwa muda mrefu.
"Wananchi wangu nawaomba tuzingatie kuchangia kile kiasi ambacho
kimepitishwa ili kuwezesha kupata asilimia 2.5 ya fedha za mradi, fedha
hii haiendi sehemu nyingine itawasaidia kukarabati miundombinu yenu ya
maji ili msipate tena shida ya maji, kwani mkishakabidhiwa mradi nyie
wenyewe ndio wasimamizi wakuu," alisema Jafo.
Katika miaka mitatu ya uongozi wa Jafo katika jimbo hilo, vijiji 11
vimeanza kupata huduma ya maji karibu na maeneo yao huku zahanati 11
zikijengwa kupunguza umbali wa wananchi kutembea kufuata huduma za
afya.
Chanzo; Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment