Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
HALMASHAURI
ya Mji wa Kibaha, mkoani Pwani, imeanzisha Chama cha Akiba na Mikopo
SACCOS ya Vijana inayoitwa Kibaha Mji Vijana Saccos Ltd, ambayo
ilizinduliwa na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu, Bi.
Rachel Kassanda.
Akiwasilisha taarifa ya
uanzishaji wake, Katibu wa SACCOS hiyo Bi.Rachel Jacob, alisema
imesajiliwa mwaka 2013 kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika namba
20 ya mwaka 2003, kifungu namba 27.
Alisema lengo la
kuanzishwa kwake ni kuinua kipato cha vijana kiuchumi ili kuchochea
maendeleo na kupunguza wimbi la umaskini kwa vijana katika jamii.
"SACCOS hii tayari
imeanza kubuni wazo la miradi ya kiuchumi kwa wanachama wake na
kujiandaa kuanza utekelezaji wake rasmi mapema iwezekanavyo," alisema.
Bi. Jacob alisema
miongoni mwa miradi iliyobuniwa ni uanzishwaji wa shughuli za ufyatuaji
tofali katika Kata ya Mbwawa, ufugaji kuku wa kienyeji na kilimo cha
mbogamboga kwa ajili ya kuongeza kipato cha SACCOS.
Aliongeza kuwa, hadi
sasa akiba waliyonayo ni sh. milioni 14 ambapo kati ya fedha hizo, sh.
milioni 10 zimetoka Halmashauri ya Mji na sh. 1,500,000 ni fedha kutoka
Mfuko wa Jimbo la Kibaha Mjini zilizotolewa na mbunge wa jimbo hilo, Bw.
Silvestry Koka ili kuunga mkono jitihada za vijana kujikwamua kiuchumi.
Pamoja na fedha hizo,
sh. 2,500,000 ni fedha za wanachama zilizotokana na kiingilio cha
sh.10,000, hisa sh. 5,000 na akiba sh.10,000 kwa kila mwanachama.
Akipokea hundi ya
mchango wa halmashauri yenye thamani ya sh.10,000,000, Mwenyekiti wa
SACCOS hiyo, Bw. Said Ndecha alimshukuru na kumpongeza Rais Jakaya
Kikwete kwa juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali yake katika kuwajengea
uwezo kiuchumi vijana wa Tanzania ili wakabiliane na changamoto ya
ajira.
Chanzo:Majira
0 comments:
Post a Comment