Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MBUNGE wa Kisarawe, Seleman Jafo, amewasihi wakazi wa jimbo hilo
kuzingatia uchangiaji wa mfuko wa maji ili kuwezesha miradi
inayotekelezwa kuwa endelevu na kuondokana na kero ya maji ambayo imekua
ikiwakabili kwa kipindi kirerfu.
Jafo alitoa wito huo wakati akizungumza na wananchi wa vijiji vya
Kihale, Panga la Mwingereza na Chole ikiwa ni baada ya kukagua maendeleo
ya ujenzi wa miradi ya maji inayotekelezwa katika jimbo hilo.
Alisema kuwa atashangaa kuona kuna mwananchi anashindwa kuchangia
asilimia 2.5 inayotakiwa kuchangiwa na wanakijijiji kwenye mfuko wa maji
kwani fedha hizo ndizo zitakazowasaidia kukarabati miundombinu pale
inapotokea tatizo.
Jafo alisema kuwa kamati za maji zinatakiwa kusimamia kikamilifu
uchangiaji wa fedha hizo kwani serikali haitaweza kumudu kugharamia.
"Wananchi wangu nawaomba tuzingatie kuchangia kile kiasi ambacho
kimepitishwa ili kuwezesha kupata asilimia 2.5 ya fedha za mradi, fedha
hii haiendi sehemu nyingine itawasaidia kukarabati miundombinu yenu ya
maji ili msipate tena shida ya maji kwani mkishakabidhiwa mradi nyie
wenyewe ndio wasimamizi wakuu,"alisema Jafo.
Alisema mradi unaotekelezwa umegharimu kiasi cha sh. milion 270 na
maji yanaanza kutoka wiki hii, hivyo ni vema kila mwananchi akawa mlinzi
wa miundombinu ya maji ili kuepusha wizi wa miundombinu.
Wakazi wa kijiji cha Kihale walikua wakitembea umbali wa kilomita 7
hadi 10 kufuata huduma ya maji, hivyo kukamilika kwa mradi huo
kutawasaidia kuachana na adha hiyo.
Baadhi yao, Zainab Hamis, Mwanahawa Juma na Hamisi Athumani,
walimshukuru mbunge huyo kwa jitihada zake zinazoendelea kutatua
changamoto ya maji katika vijiji vya jimbo.
Katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Jafo, vijiji 11
vimeanza kupata huduma ya maji karibu na maeneo yao huku zahanati 11
zikijengwa kupunguza umbali wa wananchi kutembea umbali mrefu kupata
huduma za afya.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment