Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mafia ni moja ya wilaya zilizoko mkoani wa Pwani. Shughuli
nyingi za kiuchumi katika wilaya hiyo zinategemea uvuvi, kilimo cha nazi
pamoja na utalii. Hata hivyo shughuli hizo hazijaweza kuondoa hali duni
ya maisha ya watu wake.
Mafia ina wakazi wapatao 46,000, kwa mujibu wa
sensa ya mwaka 2012.Wakazi wa wilaya hiyo walio wengi wanakula mlo mmoja
kwa siku, hii inatokana na wengi wao kutegemea uvuvi wa samaki pekee,
ambao kwa bahati sasa ni vigumu kuwavua kutokana na kuwepo kwa sheria
mbalimbali zinazowazuia wageni kuvua wanavyotaka kama ilivyokuwa zamani.
Baadhi ya wakazi wanasema zamani kulikuwa hakuna
ulazima wa kuomba kibali, lakini sasa mvuvi anapaswa kuomba kibali, huku
pia kukiwa na sheria kali za kumwongoza mvuvi wapi pa kuvua au wapi pa
kutovua.
Kwa sasa wilaya hiyo ina kiwanda kimoja cha minofu
ya samaki. Wakati kinajengwa, wananchi wengi wanamini kwamba wangepata
ajira, hata hivyo ukweli ni tofauti, kiwanda kina uwezo mdogo sana wa
kutoa ajira.
Mkurugenzi wa Wilaya ya Mafia, Fransic Namaumbo
anasema kiwanda hicho cha Tanpesca kinachangia Sh8.4 milioni kwa mwezi
katika wilaya hiyo kwa mwaka kama kodi.
Shughuli za uvuvi
Na maumbo anasema uvuvi wa samaki kwa ujumla unachangia pato kwa wilaya hiyo Sh129 milioni.
Kulingana na kiongozi huyo wastani wa kipato cha
mkazi wa Mafia kwa siku ni Sh1,350, kiasi ambacho baadhi ya wananchi
wanapingana nacho wakisema kuwa kwa namna wanavyoona, wananchi wengi
wana kipato kidogo zaidi ya hicho.
Wananchi wengi wanalalamika kwamba viongozi wa
wilaya hiyo hawasimamii vizuri rasilimali zilizopo. Wanadai kuwa
wanashindwa kuwaongoza vema wananchi kuelekea kwenye mafanikio.
Miundombinu mingi ni duni, huduma nyingi za afya
si bora, kiasi kwamba wilaya nzima inategemea hospitali moja tu kubwa
ambayo nayo imekuwa ikilalamikiwa kutokuwa na vifaa vya kutosha katika
kuhudumia wananchi.
Huduma za afya, elimu, maji safi na salama na
barabara ni mojawapo ya kero kubwa zilizoko katika Wilaya ya Mafia, huku
wenye madaraka wakilaumiwa kutoa ahadi nyingi zaidi kuliko vitendo.
Baadhi ya wafanyakazi wanaopangwa kufanya kazi Mafia kutoka mikoa mingine, hukimbia, kutokana na miundo mbinumingi kuwa duni.
Wilaya hiyo ina umaarufu wa kilimo cha aina mbalimbali kama cha
minazi, ambayo huingiza fedha nyingi kwa serikali ya wilaya. Kuna wakazi
wengi ambao maisha yao yanategemea kuuza nazi.
Ni kutokana na kuuza nazi, baadhi ya watu wamekuwa wakifungua miradi ya maendeleo licha ya kwamba mingi ni midogo.
Kulingana na taarifa ya wilaya hiyo, hekta 26,000
za ardhi zinatumiwa kwa kilimo cha minazi, mingi ilipandwa muda mrefu
sana. Baadhi ya minazi hiyo haizai na kilimo chake siyo cha kisasa.
Kwa sasa Mafia kuna minazi 52,000 inayozalisha
tani 32 hadi 34,000 za nazi kwa mwaka na kila nazi moja huuzwa Sh300,
hii ikiwa na maana kuwa kwa biashara ya nazi pekee huingiza wastani wa
Sh4.8bilioni kwa mwaka.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wanasema biashara
hiyo imekuwa haina msaada mkubwa kwa wakazi wa kawaida kwa vile walio
wengi huuza nazi moja au chache. Wenye kupata faida kubwa ni wale
wanaonunua nazi nyingi kwa wananchi na kwenda kuziuza kwa jumla.
Wafanyabiashara hununua kwa bei waitakayo, hata
chini ya Sh300, licha ya ukweli kwamba walio wengi huwa wanakwenda kuuza
hadi Sh500 kwa nazi.
Halmashauri hutoza gunia moja la nazi kwa ushuru
wa Sh1000; gunia huwa na wastani wa nazi 200 hadi 300. Licha ya kuwa na
wingi wa nazi. Mafia hakuna kiwanda cha kutengeneza mafuta ya nazi wala
tui linalotokana na nazi.
Nje ya zao la nazi, hekta 240,200 hutumika kwa
ajili ya kilimo cha mazao ya mpunga, mahindi, mihogo, ndizi mazao ya
kunde viazi vitamu, nyanya, mtama, michungwa, miembe, korosho na mboga.
Kwenye ushuru wa mazao mbalimbali ya kilimo mwaka
2011/2012 halmashauri ilikusanya Sh25 milioni. Mwaka 2012/2013
ilikusanya Sh38 milioni ikiwa ni sawa na asilimia 126 kutoka kwenye
lengo la kukusanya Sh30milioni.
Mwaka huu makisio ni kukusanya Sh30 milioni na
hadi kufikia Februari walikuwa wamepata Sh18 milioni, sawa na asilimia
62 ya lengo.
Aidha kupitia leseni za uvuvi halmashauri katika
mwaka 2011/2012 ilipata Sh50 milioni, japo makisio yalikuwa ni kupata
Sh42 milioni.
Fedha hizo zimetumika kujenga barabara, kujenga
zahanati nne ambazo mpaka sasa zipo katika hatua za mwisho na kuwekwa
vifaa na wahudumu, pamoja kununua dawa katika hospitali ya wilaya.
Hata hivyo, wananchi wengi wanaomba Serikali iwaangalie kwani wana hali duni mno kiuchumi, licha ya halmashauri kutangaza kukusanya fedha nyingi.
Chanzo:Mwananchi
Hata hivyo, wananchi wengi wanaomba Serikali iwaangalie kwani wana hali duni mno kiuchumi, licha ya halmashauri kutangaza kukusanya fedha nyingi.
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment