Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Hifadhi ya Taifa ya Saadani iliyopo wilayani Bagamoyo Mkoa wa
Pwani imeingia katika mgogoro na Kitongoji cha Uvinje kilichomo ndani ya
hifadhi hiyo.
Kitongoji hicho, ambacho ni kati ya vitongoji nane
vya Kijiji cha Saadani, kilitakiwa kiondolewe tangu mwaka 2005 baada ya
hifadhi hiyo kupandishwa daraja kutoka pori la akiba na kuwa hifadhi
kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Namba 281 la Septemba 16, 2005.
Hata hivyo wananchi wa kitongoji hicho wanadai
kuwa Rais Jakaya Kikwete alifika kijijini hapo kabla ya kuingia Ikulu na
kuwahakikishia kuwa hawataondolewa.
Maelezo ya wananchi
Wakizungumzia mbele ya watafiti wa Taasisi ya Haki
Ardhi iliyotembelea kijiji hicho hivi karibuni, baadhi ya wananchi
walisema kuwa kitongoji hicho kimekuwapo kwa muda mrefu na waliishi bila
bughudha hadi pori hilo lilipobadilishwa na kuwa Hifadhi ya Taifa.
Waliongeza kuwa, hata wakati Rais Jakaya Kikwete
alipokuwa mbunge wa Chalinze aliwatembelea mwaka 2005 na kusisitiza kuwa
hawataondolewa.
“Wakati hili ni pori la akiba tuliishi vizuri tu
na wazazi wetu walikuwa ni wafanyakazi wa pori. Lakini tangu iwe hifadhi
imekuwa taabu. Sasa tunafukuzwa wakati tumezaliwa hapa na wazazi wetu
wamezikwa hapa hapa,” anasema Hassan Akida.
Naye Zam Juma anaongeza kusema: “Rais Kikwete
alikuja hapa muda mfupi kabla hajagombea urais mwaka 2005. Tena walikaa
hapo (anaonyesha kwa kidole). Aliuliza maswali kuhusu huu mgogoro.
Wataalamu kutoka Tanapa walimweleza yote, likiwamo hilo tangazo katika
gazeti la Serikali.”
“Alisema, hawa watu msiwatishe, msiwapige kwa
bunduki, mahali hapa ni pao. Lakini tunashangaa bado Tanapa
wanatufuatilia tu. Malalamiko yetu yako wilayani, mkoani hadi Ikulu.”
Kuhusu uongozi wa Wilaya ya Bagamoyo na Mkoa wa
Pwani, Akida anasema awali walishapitisha azimio la kutokiondoa
kitongoji hicho, huku mkuu wa wilaya wa sasa, Ahmed Kipozi akidaiwa
kupinga.
“Wakuu wa wilaya waliopita hapa kama Grace Misaki,
Hawa Ngulume, Selengo Mulengo na Magesa Mulongo na aliyekuwa mkuu wa
mkoa, Dk Christine Ishengoma (sasa mkuu wa mkoa wa Iringa) walisema hili
eneo ni letu. Waliagiza kwa barua kuwa tusihamishwe,” anasema Akida.
Hata hivyo mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed
Kipozi na Mkuu wa mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma walipotafutwa
kuzungumzia suala hilo walisita kutoa maelezo.
Wakati mgogoro huo ukiendelea wakazi wa kitongoji hicho wamekiri
kumpokea mwekezaji kutoka Uingereza aliyetajwa kwa jina la Bernard
Bochad anayejiandaa kujenga hoteli ya kitalii katika eneo hilo.
Saadani wafafanua
Akizungumzia suala hilo, mhifadhi mkuu wa Saadani,
Hassan Malungu amesisitiza kuwa kitongoji hicho kimo ndani ya hifadhi
kinyume cha sheria na kwamba mambo ya siasa ndiyo yamechelewesha
kukiondoa.
Alisisitiza kuwa sheria za hifadhi za Taifa haziruhusu makazi ya watu ndani yake.
“Kwa ufupi tu ukiangalia GN (Tangazo la Serikali)
linaonyesha kuwa eneo lote la kitongoji cha Uvinje liko ndani ya
hifadhi. Ni kweli lilikuwa eneo la watu ambao walikuwa watumishi wa pori
la akiba tangu lilipoanzishwa mwaka 1968. Waliombwa kuondoka lakini
waliendelea kuongezeka,” anasema.
“Hata wakati pori hili linabadilishwa kuwa hifadhi
mwaka 2005, walikabidhi lakini wakasema kuna watu ndani. Sasa watu wa
hifadhi wako makini zaidi na sheria, lakini kila wakitaka kuwaondoa
kunakuwa siasa zinaingilia. Watu wakitaka madaraka ndiyo inakuwa hivyo…
kwa hiyo siasa ndiyo zinachelewesha jambo hili,” alisema.
“Wakati nakuja hapa nimesikia kwamba wakati
anafanya kampeni mwaka 2005, Rais Kikwete alipangiwa ratiba ya
kutembelea kitongoji hicho. Lakini kwa kujua mgogoro huo, alisita ila
hakuwa na la kufanya. Alipofika kule aliwaambia wakazi hao kuwa hata
wakiondolewa, atahakikisha kuwa wanafaidika.”
Malungu aliongeza kuwa aliwahi kumuuliza mkurugenzi wake kuhusu msimamo wa Rais kwa mgogoro huo.
“Alinijibu kuwa Rais hajakataa watu kuondoka, ila
anataka tumjengee kila mtu nyumba yake na tuwape fedha za kuanzia
maisha. Sasa tukasema hii tutaifanyaje? Maana fidia ina taratibu zake,
tutaibebaje hiyo?”
Anasema katika makubaliano, iliamuliwa kuwa
walipwe fidia kwa taratibu za Serikali na isiwe chini ya Sh3 milioni kwa
kiwango cha chini na kiwango cha juu kiwe Sh5 milioni, kulingana na
eneo la mtu.
Hata hivyo, anasema licha ya kutekeleza utaratibu wa fidia bado wamegoma kuipokea mbali ya wachache kujitokeza.
“Tulifanya utaratibu ikiwa pamoja na kuandaa
fidia. Watu walijitokeza pale kijijini kama 16 wakisema kuwa wako
tayari. Siku ya kufanya tathmini tuliishirikisha Idara ya Ardhi, baadhi
yao walikataa,” alisema Nguluma na kuongeza:
“Hiyo ilikuwa ni mwaka 2011 wakati wanakijiji walipowatishia
wathamini, ikabidi mkuu wa wilaya awape ulinzi wa polisi. Hata hivyo
ilishindikana kwa kuwa mwenyekiti wa kitongoji hakutoa ushirikiano wa
kuonyesha maeneo ya watu.”
Anasisitiza kufuatwa kwa sheria za hifadhi licha ya kujua umuhimu wa uhusiano na wananchi wanaozunguka.
“Tuko makini sana kwenye sheria. Tangazo la
Serikali likisema hivi, kwa kweli ndiyo tunavyofuata. Mipaka hii ndivyo
ilivyowekwa, huwezi kulalamika tu. kama wanataka wapeleke bungeni
ibadilishwe,” anasema.
Kauli ya Serikali
Licha mgogoro huo kuwepo kwa muda mrefu, Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka amesema
bado mgogoro huo haujafika mezani kwake bali anachokijua ni mgogoro kati
ya hifadhi hiyo na shamba la Agro EcoEnergy.
“Hiyo kesi bado haijafika mikononi mwangu. Wailete
tu niwasikilize. Ninachokijua ni mgogoro kati ya Saadani na Agro
Ecoenergy ambao nilishasema kuwa watu wa hifadhi walikosea kubadilisha
matumizi ya shamba la Razaba la Zanzibar na kuwa hifadhi na
tumeshawaambia Wizara ya Maliasili na Utalii.”
Shamba la Razaba lililokuwa mali ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar lilichukuliwa na Serikali ya Muungano na
kukabidhiwa kwa kampuni ya Agro Ecoenergy mwaka 2006.
Hata hivyo, kaimu mkuu wa Idara ya Ardhi,
Maliasili na Mazingira wa Wilaya ya Bagamoyo, Clemence Mkusa alisema
kuna kamati ya wilaya iliyokuwa ikiushughulikia mgogoro huo na kwamba
tayari wameshapeleka taarifa katika Wizara za Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi na Wizara ya Maliasili na Utalii.
“Ni kweli huo mgogoro upo. Tunayo ramani
inayoonyesha kuwa kitongoji cha Uvinje kiko ndani ya hifadhi na
wanakijiji wanatakiwa waondoke. Tumeshapeleka mapendekezo yetu wizarani
kwamba wafidiwe waondoke au wapewe hisa ya hifadhi hiyo. Tunasubiri
majibu,” alisema Mkusa.
Naye mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori wa Wizara
ya Maliasili na Utalii, Paul Sarakikya alikiri kuufahamu mgogoro huo na
kusema kuwa kwa sasa kuna timu ya Waziri Mkuu iliyoundwa kushughulikia
migogoro ya ardhi katika hifadhi zote nchini.
“Tusubiri tu hadi watakapotoa taarifa yao,” anasema Sarakikya.
Hifadhi ya Taifa ya Saadani;
Saadani ni hifadhi pekee ya Taifa nchini na Afrika Mashariki
yenye fukwe za bahari na inayotazamana na Bahari ya Hindi na fukwe zake
zinakutana na uoto wa asili wa nchi kavu.
Inapatikana katika mikoa ya Tanga na Pwani. Uwepo
wake ni matokeo ya pori la akiba la Saadani, ranchi ya Mkwaja na sehemu
ya kaskazini, sambamba na akiba ya msitu wa asili wa Zaraninge.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment