Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, mkoani
Pwani, limemtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda kumtafutia kituo kingine cha
kazi Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Samweli Sarianga, kutokana na
kushindwa kutimiza majukumu yake.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao cha Baraza la
Madiwani hivi karibuni, Mwenyekiti wa baraza hilo, Shukuru Mbatto,
alisema wamemuomba Waziri Mkuu kumtafutia kituo kingine mkurugenzi huyo
kutokana na kushindwa kuonyesha ushirikiano kwa madiwani.
Alisema sababu nyingine ni kushindwa kutimiza majukumu yake na
kuwasimamia watendaji walio chini yake katika kituo chake cha kazi.
Mwenyekiti huyo alisema kwa muda mrefu madiwani hao wameshaandika
barua kadhaa kwenda Ofisi ya Waziri Mkuu na Mkuu wa Mkoa wa Pwani,
kuingilia kati mgogoro uliopo baina ya madiwani na mkurugenzi huyo, ili
kuweza kutekeleza miradi ya maendeleo kama ilivyopangwa.
Awali katika kikao hicho, madiwani hao walikataa kupitisha taarifa ya
robo ya tatu ya mapato na matumizi ya halmashauri hiyo mwaka 2012/13
kwa madai kuwa imejaa ufisadi na kuiomba Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa
Pwani kutuma timu ya wakaguzi, ili kufanya ukaguzi wa hesabu kwenye
halmashauri hiyo.
Mbatto aliongeza kusema kilichofanywa na watendaji wa halmashauri
hiyo ni dharau, kwani pamoja na madiwani kugomea taarifa hiyo katika
kikao kilichowahi kufanyika huko nyuma, bado taarifa imewasilishwa
mbele ya kikao hicho ikiwa imevurugwa na kujaa shaka.
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Sarianga alikiri kuwapo kwa makosa
katika taarifa hiyo na kuwaomba radhi madiwani hao na kuahidi kuangalia
makosa yaliyopo na kuifanyia marekebisho.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Sarianga ilikataliwa na madiwani hao ambao
walisisitiza kutumwa kwa wakaguzi maalumu kutoka Ofisi ya Katibu Tawala
kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa fedha za miradi na mapato na matumizi
ya halmashauri hiyo kabla ya madiwani hao hawajamchukulia hatua.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment