Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mtoto wa marehemu aliyeokolewa katika ajali hiyo akiwa na shangazi yake
Mvua inaweza kuwa neema pale inaponyesha kwa
wastani, lakini ikawa karaha pale inapokuwa kubwa, hasa kwa watu
wanaoishi mabondeni au kandokando ya mito.
Mikoa mingi nchini imepata adha ya mafuriko
kutokana na mvua zilizoanza kunyesha mwezi uliopita. Lakini kwa wakazi
wa vijiji vilivyopo kandokando ya Mto Rufiji, mvua zimewaletea wageni
hatari katika maeneo yao.
Wageni hawa ni viumbe hatari; ni mamba
waliowageuza wenyeji wao kuwa kitoweo na kuwafanya waishi kwa wasiwasi
wakihofia usalama wao.
Wakazi hawa wanashindwa kuendelea na maisha yao
kama kawaida, ikiwemo shughuli za kilimo ambazo huzifanyia ng’ambo au
pembezoni mwa mto huo.
Kwa muda mrefu sasa mnyama huyo amekuwa tishio kwa
wakazi wa Wilaya ya Rufiji. Wanyama hao wengi huishi katika mabwawa
yaliyopo katika Hifadhi ya Selous, lakini mvua inaponyesha na maji
kujaa mtoni, mamba hurahisishiwa kazi ya kuwinda binadamu.
Wakazi wa vijiji vya Utete, Chemchem, Mkongo,
Ngorongo, Nyaminywili, Mloka na Mwaseni hujishughulisha na kilimo cha
mazao ya mahindi, mpunga, ndizi na matikitimaji kando ya mto huo.
Wengi wao hulazimika kuvuka mto huo ili kwenda
ng’ambo ya pili kulima, au kuwinda ndege na usafiri wao mkubwa ni
mitumbwi ambayo siyo salama katika kipindi hiki.
Hivi karibuni, mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi
tawi la Lumumba katika kijiji cha Kilimani Mashariki, Saidi Simba (60)
aliliwa na mamba wakati akivuka mto huo.
Akiwa na mwanawe wa kiume, Seif Saidi (5) mtumbwi waliokuwa wakisafiria ulijaa maji na kumlazimu kushuka ili ayaondoe.
Aliposhuka tu alipokelewa na mamba ambaye
alimzamisha na kutoweka naye huku mtoto wake akibaki na taharuki na
kulazimika kupiga kelele kuomba msaada.
Ofisa mtendaji wa Kijiji cha Kilimani Mashariki,
Masudi Mminge anasema kuwa katika eneo hilo, mamba huweka makazi hasa
wakati wa mvua.
Anasema tatizo la wanyama hao ni kubwa katika kijiji chake na vijiji vya jirani, hasa katika kipindi cha masika.
Anasema kuwa mamba hao wakishaona maji yamekuwa mengi nao
hutumia mwanya huo kutafuta chakula karibu na makazi ya watu au
mashamba.
Mminge anasema kuwa maeneo alipozama marehemu Simba kuna mamba wengi wenye urefu wa hadi futi 15.
“Juzi tu hapa wamekamata ndama wa mfugaji mmoja ambaye aliwapeleka kunywa maji,” alisema.
Dada wa marehemu, Khadija Ali anasema marehemu
kaka yake aliagiza familia nzima kwenda shambani kwa ajili ya kuhamia
ndege na wanyama wengine waharibifu wa mazao.
Anasema alitanguliwa na mtoto wake Seif, huku
baadhi ya ndugu na wake zake wakiwa nyuma kwenda katika mashamba kwa
ajili ya kulinda shamba dhidi ya ndege na wanyama.
“Alitangulia katika mtumbwi mdogo na sisi ilikuwa
tupande mwingine, lakini kwa bahati mbaya alichukuliwa na mamba na mpaka
sasa hatujaupata mwili wake,” anasema Khadija.
Mtoto Seif Saidi (5) anasema kuwa aliondoka na
baba yake wakiwa na chakula, makuti kwa ajili ya kujengea dungu (aina ya
nyumba) na jamvi.
Anasema kuwa alipoona baba yake anazama, alianza kupiga kelele za kuomba msaada lakini hakuuona tena mwili wa baba wake.
“Nilimwona akivutwa kwa nguvu na hakuibuka tena, nilipiga kelele kuomba msaada. Nasikitika sijamuona tena baba yangu,” anasema.
Kwa upande wake, Hamisi anasema kuwa baada ya
kusikia kelele za kuomba msaada, naye alipiga kelele watu wakaongezeka
na kuingia katika mkondo huo kwa mitumbwi na kufanikisha kumuokoa mdogo
wake.
Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Ali Mwegio
aliyeoongoza kikosi cha uokoaji kwa kutumia mitumbwi eneo hilo, anasema
kuwa wametafuta mwili wa marehemu bila mafanikio.
“Kuna kipindi tulikuwa tukisikia harufu kali
tukaaamini kabisa ni ndugu yetu mpendwa, lakini eneo panaposikika harufu
hiyo kuna mamba wengi, tumeshindwa kusogelea eneo hilo kwa sababu ya
usalama wetu,” alisema.
“Mamba akishakuchukua, hukuficha kwanza halafu ukioza ndio hula nyama,” alisema Mwegio.
“Mamba akishakuchukua, hukuficha kwanza halafu ukioza ndio hula nyama,” alisema Mwegio.
Uamuzi wa Serikali
Ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Masudi Mminge
anasema kuwa hatua ya kwanza aliyochukua kama Serikali ni kuwatangazia
wananchi kutokwenda mabondeni kipindi hiki cha mvua.
Anasema kuwa wakazi hao wasiende kabisa maeneo ya
bondeni katika kipindi hiki cha mvua kubwa, licha ya kwamba wanatakiwa
kwenda kwa ajili ya kulinda mazao yao.
Mminge alisema kuwa anatambua kuwa uwezekano wa
wakazi hao kunyemelewa na njaa ni mkubwa, lakini amechukua tahadhari
mapema kwa kuanza kutembelea kaya ambazo anaona ziko katika hatari ya
kukumbwa na njaa.
Hatua ya pili ni kwamba mbunge wa Jimbo la
Rufiji, Dk Seif Rashid ambaye ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii
alifika katika msiba wa Said Simba ambapo wananchi wamemuomba asaidie
kuwapatia mtumbwi mkubwa utakaosaidia kuwavusha wananchi hao kuvuka
vijito vinavyounganisha mto.
Anasema kuwa wakazi wa maeneo hayo hawavuki Mto
Rufiji bali wanalima pembeni mwa mto huo, ambao ukifurika maji mamba
huzagaa hadi katika mashamba yao wameomba mtumbwi mkubwa wa kuwasaidia
kuvuka vijito, jambao ambalo waziri huyo ameahidi kulifanya.
Matukio ya mamba kula watu
Ni matukio ya kawaida kama anavyosimulia meya wa
mji mdogo wa Utete, Masudi Jaha anayesema kuwa wakazi wa wilaya hiyo
waache mazoea ya kuamini kuwa maji wameyazoea.
Aliyekuwa diwani wa Kata ya Mgomba wilayani
hapa kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Kasimu Mlekeni alinyofolewa tako
la kulia na mamba wakati akioga katika dimbwi lililopo karibu na shamba
lake lililopo eneo la Nyamaruba.
“Kumbukumbu zangu zinaonyesha kuwa kila mwaka mamba anakula mtu, lakini watu wengi hupotea zaidi ya ninavyofahamu,” alisema Jaha
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Nurdin Babu anasema
kuwa Mto Rufiji umefurika na maji ni mengi mno na kwamba mafuriko hayo
yameharibu mazao mashambani na hivyo kukwamisha mawasiliano kati ya kata
moja na nyingine.
Babu anasema kuwa baadhi ya makazi ya watu katika eneo la Daraja
la Mkapa yamemezwa na maji, hivyo kuhatarisha usalama wa wananchi
wanaoishi mashambani na kuwataka kuwa waangalifu katika maeneo yao.
Anasema kuwa maeneo hayo yanafuga mamba wengi na
wakati kunapotokea mafuriko, mamba hao huzagaa kila mahali kwa lengo la
kutafuta chakula na hivyo amewaomba wakazi hao kuchukua tahadhari
hususan wanaokwenda kuvua, kuogelea na kuteka maji.
“Sisemi msiende mtoni lakini mchukue tahadhari
hasa kipindi hiki kigumu cha mafuriko kuna mamba wengi jamani,”anasema
na kuongeza katika kipindi cha Januari hadi sasa watu wanne
wamechukuliwa na mamba na hadi leo hawajaonekana.
Anaongeza kuwa katika kipindi cha Januari hadi
mei, jumla ya watu wanne wamechukuliwa na mamba na mpaka sasa miili yao
haijapatikana.
“Kutokana na maji kuwa mengi ni vigumu kuipata
miili ya watu wanaochukuliwa na mamba, ndio maana ninawasihi watu waache
tabia ya kukaribia mto huu,” anasema Babu.
Athari za mafuriko
Babu anasema kuwa mafuriko yamesababisha hasara
kubwa kwa mazao mashambani na wapo katika mchakato wa kujua ni kaya
ngapi zimeathirika na mafuriko ili watume taarifa ofisi ya waziri mkuu
kitengo cha maafa kwa ajili ya msaada wa chakula.
Pia anasema kuwa mawasilino kati ya baadhi ya kata na kata vijiji na vijiji yamekatika kutokana na makaravati kusombwa na maji.
Anasema kuwa hakuna mawasiliano kati ya Kata ya
Ngorongo na Mwaseni, huku maeneo mengi yakijaa maji jambo ambalo
limewafanya wakazi kukwama kufika katika baadhi ya maeneo.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment