Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
RIDHIWANI Kikwete, Mbunge Mteule wa Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani amesema kuwa yeye ni mbunge wa watu wote wa Jimbo la Chalinze.
Alisema imani waliyompa wananchi wa Jimbo la Chalinze kwa kumpa kura nyingi na kuwa mbunge wa jimbo hilo, ataifanyia kazi kwa kuwa mbunge wa watu wote kwa kushirikiana kwa kila jambo la maendeleo.
Ridhiwani alisema hayo jana katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wenye lengo la kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Chalinze kwa kumchagua Ridhiwani kuwa mbunge wa jimbo hilo.
Alisema amefanya kampeni kwa mwezi mmoja na amepita katika vijiji vyote 81 vya Jimbo la Chalinze na amejua kila changamoto zilizoko katika jimbo hilo, hivyo kazi aliyonayo ni wananchi kumuamini na kumpa ushirikiano kwani atafanya kazi na kila mtu wa jimbo hilo.
Ridhiwani alisema atafanya kila jambo aliloahidi kwa kasi kubwa kwa kushirikiana na wananchi na viongozi wa serikali wa ngazi zote kwa maslahi ya wananchi wa Chalinze.
‘’Mimi ni mbunge wa watu wote hapa Chalinze na sitafanya kazi kwa kubagua ama kwa ukabila au kwa makundi kwani nimechaguliwa na wananchi wa Jimbo la Chalinze wa rika zote,’’ alisema.
Katika uchaguzi huo mdogo, jimbo hilo limepata wapigakura wengi kuliko majimbo yote yaliyowahi kufanya uchaguzi mdogo hapa nchini tangu mwaka 2010.
Imeelezwa kuwa kura 20,828 alizopata Ridhiwani, mgombea wa CCM ni sawa na asilimia 86.6 na zimevunja rekodi ya nchi nzima kwenye uchaguzi mdogo.
Katika matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa majira ya saa 8.40 usiku wa jana, Ridhiwani wa CCM alipata kura 20,828; mgombea wa Chadema, Mathayo Torongey alipata kura 2,244 sawa na asilimia 10.5 na mgombea wa CUF Fabiani Skauti aliambulia kura 476 sawa na asilimia 1.9.
Wagombea wengine waliokuwa wakiwania kiti cha ubunge katika Jimbo la Chalinze ni pamoja na Ramadhani Mgaya aliyepata kura 78 sawa na asilimia 0.32 na Husseni Munir aliambulia kura 60 sawa na asilimia 0.24.
Ushindi wa Ridhiwani ulianza kuonekana mapema tangu hatua za awali za kampeni hizo ambazo zilianza Machi 14 mwaka huu ambapo alikuwa akijaza wasikilizaji kwenye mikutano ya kampeni ya chama chake ukilinganisha na mpinzani wake mkubwa wa CHADEMA, Mathayo Torongey.
Akitangaza matokeo hayo msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Samwel Salianga ambaye pia ni mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo, alisema kuwa wakazi walioandikishwa kwenye daftari la wapiga kura walikuwa zaidi ya 92,000 ambapo waliopiga kura kwenye uchaguzi huo walikuwa 24,422 ambapo uchaguzi wa 2010 waliopiga kura ni zaidi ya 36,000.
Salianga alisema kuwa watu waliojitokeza kupiga kura ni wachache ikilinganishwa na wale waliojiandikisha kwenye daftari la wapiga kura, hata hivyo hakuweza kusema ni changamoto gani iliyosababisha idadi ya wapiga kura kuwa ndogo.
“Mwamko umekuwa ni mdogo licha ya kutolewa kwa matangazo na elimu juu ya umuhimu wa zoezi la kupiga kura na faida zake, lakini bado watu hawajaona umuhimu wake, hali ambayo inawafanya wakose haki yao ya msingi ya kushiriki uchaguzi,” alisema Salianga.
Uchaguzi huo mdogo wa Jimbo la Chalinze ulifanyika kutokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Said Bwanamdogo kufariki dunia mwanzoni mwa mwaka huu, hali iliyosababisha kuzibwa kwa nafasi hiyo.
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment