Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
DIWANI wa Shume, Rashird Kisimbo, amelitaka Jeshi la Polisi nchini
kuwakamata na kuwafungulia mashitaka ya mauaji askari wake sita wa
Kituo cha Polisi Lushoto wanaotuhumiwa kumuua raia mmoja na kujeruhi
mwingine.
Askari hao wanatuhumiwa kumuua kwa risasi, mkazi wa Kijiji cha Viti,
wilayani hapa, Hamis Seif (25) na kumjeruhi Athuman Mgazija
wakiwatuhumu kuwa ni majambazi.
Chanzo cha mauaji hayo ni hatua ya askari hao kuvamia nyumba ya
Mohamed Hamis, saa tano usiku wakidai kutekeleza amri ya Mahakama ya
Wilaya ya Korogwe kwa kile walichodai mwananchi huyo alipuuza wito wa
mahakama hiyo katika shauri la madai.
Uchunguzi uliofanywa na timu ya waandishi wa habari za uchunguzi
wilayani hapa kwa wiki mbili, umebaini tikio hilo lilitokea Oktoba 17
mwaka jana, lakini hadi sasa limefanywa siri na mamlaka husika, ikiwamo
kushindwa kuwawajibisha askari waliohusika na mauaji hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, diwani huyo alihoji
ukimya wa Jeshi la Polisi kutowakamata askari hao huku wakihamishiwa
vituo nje ya Wilaya ya Lushoto.
Diwani huyo aliungana na wananchi hao kukanusha madai ya askari hao
kuwa waliowavamia na kuwashambulia walikuwa ni majambazi, na kusema
askari hao walivamia nyumba ya mwananchi huyo bila kushirikisha uongozi
wa ngazi zote kuanzia kitongoji, kijiji hadi kata.
Alisema kuwahamisha vituo na kuwashusha vyeo askari hao si suluhisho
na hakuondoi uhalisia wa tukio hilo, huku akitupia lawama uongozi wa
Serikali ya Wilaya ya Lushoto kwa kutoingilia kati tukio hilo.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment