SERIKALI wilayani Mkuranga, Pwani, imeombwa kutoa elimu ya sehemu
sahihi ya kufikisha migogoro ya ardhi na namna ya kuitatua, ili
kupunguza wimbi la migogoro hiyo.
Ombi hilo lilitolewa mwishoni mwa wiki na baadhi ya wakazi wa
Mkuranga baada ya kupatiwa mafunzo ya sheria namba saba ya mabaraza ya
kata ya mwaka 1985 na Asasi isiyo ya Kiserikali ya Ushirikiano wa
Vijana wa Mwandege (USHIVIMWA).
Akizungumza baada ya mafunzo hayo, mmoja wa washiriki hao, Shwaari
Maneno, alisema wananchi wanatakiwa kupatiwa elimu hiyo ili waweze kujua
sehemu sahihi ya kupeleka migogoro yao.
Veronika Mloka mjumbe wa baraza la kata ya Kiparang’anda alisema
migogoro mikubwa katika maeneo yao ni ya ardhi ambayo wakati mwingine
inatishia amani kwa walengwa.
Mloka aliiomba serikali kufikisha elimu kwa wananchi na viongozi wa
mabaraza, ili migogoro hiyo imalizike katika ngazi ya kata badala ya
hali ilivyo sasa ya kuifikisha polisi na kurudi tena kata hali
inayochangia kutumia muda mwingi.
“Kabla ya kushiriki mafunzo haya sikujua namna ya kuendesha mabaraza
wala kuwaelekeza wananchi waanzie wapi wanapokua na kesi kama hii sasa
nitatoa elimu hii kila utakapofanyika mkutano ili wananchi waelewe,”
alisema.
Katibu Mtendaji wa Asasi hiyo, Nuri Kiswamba, alisema wamefikia hatua
ya kutoa mafunzo hayo baada ya kuona ongezeko kubwa la migogoro ya
ardhi katika maeneo mbalimbali.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment