Home » » TASJA yataka Saadani kutunza mazingira

TASJA yataka Saadani kutunza mazingira

CHAMA cha Waandishi wa Habari za Sayansi (TASJA), kimewataka wakazi wanaoishi eneo la Hifadhi  ya Saadani, kuhifadhi mazingira ya Mbuga hiyo ili iweze kuendelea kuwa historia hadi katika vizazi  vijavyo.
Mwenyekiti wa Chama hicho, Gryson Mutembei, alitoa wito huo hivi karibuni, wakati wa ziara ya chama hicho katika hifadhi hiyo iliyolenga kujifunza mazingira na viumbe hai.
Katika ziara hiyo iliyowezeshwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) na kutanguliwa na semina ya siku mbili, Mutembei alisema baada ya mafunzo wamegundua jinsi mazingira na viumbe hai vinavyotegemeana, hivyo kama wakazi hao hawatatunza mazingira, hata wanyama hawatakuwepo.
David Ramadhani ni mmoja wa wanachama wa TASJA, alisema hakujua kama Tanzania ina vivutio vizuri kama Saadani ambayo ni mbuga pekee inayokutanisha bahari na mto, jambo linalofanya watalii wengi kwenda kuangalia.
Kutokana na hilo, Ramadhani alisema safari za waandishi ni muhimu mara kwa mara katika vivutio hivyo kwa sababu wataweza kutumia kalamu zao kuvitangaza na kuvifanya vijulikane dunia nzima.
Mhifadhi Idara ya Ulinzi, Ismail Omar, alisema wamekuwa wakianzisha miradi mbalimbali kwa wananchi kama mbadala wa kutowinda wanyama kwa ajili ya kitoweo.
Omar alisema kumekuwepo na mahusiano mazuri ya kupata ujirani mwema na wananchi ikiwemo katika kushiriki shughuli mbalimbali za  maendeleo
Chanzo;Tazania daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa