MKUU wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza, ametoa wito kwa wenyeviti wa
halmashauri zote za mkoa huo kusisitiza kilimo cha ufuta ambacho
kitakuwa mbadala wa zao la korosho linalosuasua kwa sasa.
Mahiza alitoa wito huo mwishoni mwa wiki alipozungumza na wadau
mbalimbali wa kamati ya ushauri ya mkoa huo kwenye kikao chake
kilichofanyika mjini Kibaha.
Alisema kwa sasa zao la korosho linasuasua, hivyo ni vema viongozi
wakasisitiza kilimo cha ufuta kitakachowakomboa wananchi wengi hasa
katika suala la maendeleo.
“Wenyeviti wa halmashauri himizeni kilimo cha ufuta katika maeneo
yenu, wakazanieni wananchi wenu katika suala la kilimo kitasaidia
kuwawezesha kulipa ada za watoto na kufanya mambo mengine ya
kimaendeleo,” alisema.
Aidha, alisema endapo wananchi hao watajikita katika kilimo cha zao
hilo kitawasaidia pia kulipa gharama za mfuko wa bima ya afya na
kuongeza idadi ya wananchi wanaojiunga na mfuko huo.
“Mtu akishindwa kulima ufuta basi afuge kuku; wekeni sheria za
kujiunga na mfuko wa bima ya afya, ili kila mwananchi aweze kujiunga.
Natambua hali ya uchumi ya wananchi wangu tusipowakazania katika kilimo
hakutakuwa na maendeleo,” alisema.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment