Home »
» Watumishi wa Mahakama watakiwa kufuata maadili
Watumishi wa Mahakama watakiwa kufuata maadili
JIBU LA SWALI LA MBUNGE Kibaha vijijini
|
|
|
SERIKALI imewataka watumishi wa Mahakama nchini ambao hawataki
kufuata sheria, kanuni na maadili ya kazi yao kuondoka mara moja
kazini.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Katiba na
Sheria, Angellah Kairuki, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge
wa Kibaha Mjini, Silvester Koka (CCM), aliyetaka kujua mkakati wa
serikali katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili watendaji wa
mahakama, ikiwamo ukosefu wa nyumba, sare na masilahi duni
yanayochangia kupokea rushwa.
Katika swali lake la msingi, mbunge huyo alitaka kujua mpango wa
serikali katika kujenga jengo jipya la Mahakama ya Mwanzo kwenye
Halmashauri ya Mji wa Kibaha, ili iweze kutoa huduma zake sawasawa.
Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Karatu, Israel Naste (CHADEMA),
alitaka kujua nini kimetokea katika maendeleo ya ujenzi wa Mahakama ya
Wilaya ya Karatu ambao ulikuwa ukienda kwa kasi na kwa sasa umesimama.
Akijibu maswali hayo, naibu waziri huyo alisema tayari
wameshawasiliana na wasajili wa wilaya wa Mahakama kupata orodha ya
watumishi wanaohitaji sare na kuongeza kuwa changamoto ya nyumba na
masilahi vinashughulikiwa.
Alisema azima ya serikali ni kuona watumishi wote wa Mahakama wanatekeleza wajibu wao kama walivyoapa.
Pamoja na hayo, alikiri jengo la Mahakama ya Mwanzo Kibaha Maili Moja
ni bovu na tayari serikali imeshatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa
jengo hilo.
Alisema mpaka sasa taratibu za kumpata mshauri mwelekezi kwa ajili ya
usimamizi wa ujenzi wa jengo hilo zinakamilishwa ili kuwezesha ujenzi
huo kuanza mara moja.
“Ni mpango wa serikali kujenga majengo mapya katika mahakama zote
ambazo majengo yake ni mabovu na chakavu,” alisema naibu waziri huyo na
kuongeza kuwa kutokana na ufinyu wa bajeti wataendelea kujenga majengo
ya mahakama kadiri hali ya bajeti ya fedha itakavyoruhusu
CHANZO;TANZANIA DAIMA
|
|
0 comments:
Post a Comment