Home » » WABUNGE, MAWAZIRI WANAUGUA KIHARUSI SABABU YA UONGO WAO

WABUNGE, MAWAZIRI WANAUGUA KIHARUSI SABABU YA UONGO WAO

VIONGOZI wengi wakiwamo wabunge na mawaziri nchini imeelezwa wamekuwa wakipata ugonjwa wa kiharusi na hatimaye kupooza na kupoteza maisha muda mfupi toka wanapokuwa wametoka madarakani kutokana na kufanya vitendo vya udanganyifu wakati wa kujaza fomu za tume ya maadili na utumishi wa umma.

Udanganyifu huo umekuwa ukifanywa na viongozi wengi ambapo badala ya kuweka wazi mali zao,wao huamua kuwaandikisha ndugu au jamaa zao katika mali na miradi na kutokana na kutokuwa waaminifu ndugu ama jamaa hao huamua kuwadhulumu hivyo viongozi hao wanaporudi mtaani hupatwa na matatizo hayo baada ya kushtushwa na hali wanayoikuta katika miradi yao.

Hayo yameelezwa leo Nov 5 wilayani Kisarawe na Afisa kutoka Sekretarieti ya maadili ya utumishi wa umma, Zahra Guga kwenye uzinduzi wa mradi wa kutumia misingi ya utawala bora katika kupambana na mabadiliko ya tabia nchi

Uzinduzi wa mradi huo umefanyika katika kata za Chole na umelenga kutekelezwa kwenye kata tatu ikiwemo Vikumbulu na Marui wilayani Kisarawe na asasi isiyo ya kiserikali ya Guluka-Kwalala chini ya ufadhili wa shirika lisilo la kiserikali la The Foundation for Civil Socieyt kwa sh. milioni 135 kwa miaka 3.

 Ameongeza kuwa hata wabunge na wengineo wanapata stroke kwa sababu wanapomaliza uongozi na kurudi kule katika miradi anakuta mambo aidha ni mabaya sana kwa maana umefilisika au mtu aliyemkabidhi ameamua kumdhulumu hivyo kubaki anang’aa macho hana pa kukimbilia.

Guga amesema inawawia vigumu kumsaidi mbunge,Waziri au kiongozi wa namna hiyo kwa sababu yeye anakuwa amemkabidhi mali au mradi ndugu au jamaa yake kwa maandishi kabisa na hivyo kukosa umiliki halali.
 
Aidha Afisa huyo kutoka tume ya maadili ya watumishi wa Umma,amesema tatizo kubwa ambalo tume hiyo imekuwa ikikumbana nalo kwa sasa ni kutokuwapo kwa mifumo madhubuti,migongano ya maslahi,uwezo wa taasisi simamizi za maadili kifedha na rasilimali watu na mmonyoko wa maandili miongoni mwa jamii.

Kauli hiyo ya Tume ya Maadili na utumishi wa umma inakuja huku ikiwa ni siku chache tu tokea Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano Anna Makinda kueleza kukerwa na  baadhi ya Wabunge wa zamani ambao wamekuwa wakifika katika ofisi yake na kulia wakiomba kusaidiwa kutokana na kukabiliwa na maisha magumu.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa