Niliposoma Kitabu cha Sir Francis R. Burton, Zanzibar,
alichokiandika mwaka 1857, anasema aliwahi kutembelea Saadani, mji wa
kale alikokuwa anakaa Sultan Bwana Heri ambaye alishirikiana na Bushiri
bin Salim al-Harith.
Anasema aliambiwa habari za kuwapo kwa mji wa kale
uliopo Kusini mwa eneo hilo, Utondwe. Burton anasema aliwahi kusoma
kuhusu mji huo katika maandishi ya al-Masoud, msafiri maarufu sana enzi
za karne ya kumi
Al-Masoud alitembelea maeneo hayo karne ya kumi.
Na Wareno walianza kuja Pwani karne ya kumi na nne na kumi na tano. Basi
Utondwe ni miongoni mwa miji ya kale sana katika historia ya pwani
yetu.
Baada ya kusoma kitabu hicho nilifunga safari hadi
Bagamoyo, nilipowauliza watu wanaofanya kazi Idara ya Mambo ya Kale,
walisema hawajui na hawajawahi kusikia habari za mji huo. Mmoja wa watu
alisema alishawahi kusikia habari za mji huo wa kale, lakini hajawahi
kufika kwenye mji huo ingawa anasema alielekezwa ulipo.
Wazee wengi wa umri wa kati ya miaka 50 na 60,
walisema hawajawahi kuusikia. Nilipofanya utafiti kwenye mtandao wa
intaneti nikaona picha za maandishi ya Kiislamu (Islamic Inscriptions),
ambayo yaliandikwa kwenye makaburi ya Utondwe. Wazungu walishafika na
kufanyia utafiti, na kuchukua vibao hivyo vya maandishi kwenye makaburi.
Nilifunga safari kwa boda boda na kutembelea mji
huo ambao uko kilomita 50. Wenyeji wa eneo la Kitame wanalijua eneo
hilo, lakini hawajui kama paliwahi kuwa na mji. Kuna mashamba ya chuo na
mto wa maji chumvi, mkondo wa bahari kama alivyoeleza Francis Burton.
Burton alieleza kuwa eneo hilo lilikuwa likizalisha chumvi.
Nilipokuwa naangalia kwenye vichaka na vichuguu
niliona dalili za kuwa watu waliwahi kuishi hapo. Pia nilitembelea msitu
na baadaye nilitokea kwenye msikiti ambao sasa umebaki kuta tu na nguzo
za ndani. Paa hakuna, hakuna makazi ila makaburi mawili jirani, na moja
umbali wa mita kama ishirini, na mengine yamezolewa na mto unaopanuka.
Hii ni hifadhi ya historia, lakini hakuna anayeujua mji huu wa kale wa
Utondwe, wilayani Bagamoyo.
CHANZO;MWANANCHI
CHANZO;MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment