Home »
» Mapunda: UVCCM ni ya vijana wote
Mapunda: UVCCM ni ya vijana wote
|
|
JUMUIYA ya Umoja wa Vijana (UVCCM) imesema kuwa taasisi hiyo ni
ya vijana wote bila kujali chama kutokana na changamoto za vijana hao
kutatuliwa na serikali yenyewe kwa kuthamini mchango wao.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa UVCCM taifa, Sixtus Mapunda, wakati
akizungumza na wananchi wa mji wa Kibaha kwenye viwanja vya Mwendapole
ambapo alisema kuwa katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto za vijana
serikali haiangalii itikadi ya chama.
Mapunda alisema UVCCM ina mpango wa kuainisha vipaumbele vya vijana
kuwa pamoja na kuwatambua na majukumu yao ili wanapoanza utekelezaji
watambue eneo mahususi la kuanzia kuhakikisha kila kijana
anajishughulisha badala ya kuisubiri serikali kuwaajiri.
Akizungumza katika mkutano huo baada ya kusimikwa kuwa kamanda wa
vijana, mbunge wa Kibaha Mjini, Silvestry Koka, alisema ili kuwezesha
kila kijana anajiajiri mwenyewe, kuna mpango mkakati aliouandaa kwa
kugawa pikipiki kwenye kata 11 za mji huo.
Koka alisema pikipiki hizo zitagawiwa kwa uongozi wa madereva pikipiki
ulioko kwenye kata ili waitumie kwa pamoja na baadaye kununua nyingine
ili kuhakikisha kila kijana anamiliki pikipiki yake mwenyewe.
Akizungumzia suala la afya, alisema hivi karibuni anatarajia kukabidhi
vifaa tiba vyenye thamani ya sh milioni 25 katika awamu ya kwanza na
awamu ya pili vifaa tiba vitasambazwa katika hospitali na vituo vya afya
vilivyoko katika mji huo vikiwa na thamani ya sh milioni 700.
Katika mkutano huo wanachama wa CCM waliaswa kuwa na msimamo katika
chama chao na kuacha tabia ya kuyumbishwa na viongozi wa vyama vya
upinzani ambao alidai wengi hawana nia njema na wananchi.
Chanzo;Tanzania Daima
|
|
0 comments:
Post a Comment