Home » » Hospitali ya Wilaya Kisarawe yalalamikiwa kwa rushwa

Hospitali ya Wilaya Kisarawe yalalamikiwa kwa rushwa

Kisarawe mkoani Pwani
Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani imelalalamikiwa kwa kutoa huduma mbaya kwa wagonjwa, rushwa na wajawazito kutozwa Sh. 10,000  kuchangia mafuta ya gari la wagonjwa.
Malalamiko hayo yametolewa na baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo kwa Mbunge wa Kisarawe (CCM),  Selemani Jafo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika juzi mjini hapa.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Thabit Bakar (65) alidai kuwa huduma ni mbaya katika hospitali hiyo na baadhi ya watumishi wake wana lugha za maudhi kwa wagonjwa.

Bakari aliendelea kudai kuwa vilevile wagonjwa kabla ya kupatiwa matibabu wanatakiwa kwenda kununua pamba, dawa na sindano baada ya kuambiwa kuwa havipo.

“Kuna hizi dawa ambazo Serikali kila siku inatutangazia zimejaa ya Alu nazo tunaambiwa tukanunue, pia wahudumu wa afya hawatendi haki baadhi wanatutukana wana kauli mbaya sana hawa, ” alisema.

Vilevile  walilalamikia kutozwa fedha kwa ajili ya kadi na kumuona daktari kiasi cha Sh. 10,000.

Pia walisema wanaombwa rushwa ili kuhudumiwa haraka, kulazwa mgonjwa kwa Sh. 5,000 badala ya Sh.1,000, mafuta kwenye gari ya wagonjwa na michango mingine.

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Hamza Nzige alisema hajawahi kupokea malalamiko hayo na kuahidi kufuatilia.

Kwa upande wake Mbunge Jafo,  ameutaka uongozi wa hospitali  hiyo kushughulikia malalamiko hayo ili kuwaondolea kero.

Jafo alisema si mara ya kwanza kupokea malalamiko hayo na kwamba naye aliyawasilisha kwa uongozi wa hospitali hiyo lakini yamepuuzwa kwa kutopatiwa ufumbuzi.
 
CHANZO: NIPASHE



0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa