RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt Jakaya Kikwete anatarajiwa kuanza ziara ya siku sita mkoani Pwani wiki hii ambapo
pamoja na mambo mbalimbali atakayofanya pia atakabidhi gari moja la wagonjwa na
boti mbili aina ya ambulance boats kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa wa visiwani
katika Delta za mto Rufiji na kuzindua mradi wa uwanja wa ndege wa Mafia na
gati.
Katika ziara hiyo inayotarajiwa kuanza
wilayani Mafia Oktoba 3 na kuendelea wilaya zingine hadi Oktoba 9,Dkt Kikwete
pia atazindua na kuweka mawe ya msingi ya shughuli mbalimbali za kimaendeleo
katika sekta ya Elimu, Afya Viwanda na shughuli za vijana ambao wamejiajiri baada
ya kupata mafunzo kwenye kambi za maarifa.
Mkuu wa mkoa wa Pwani,Hajat Mwantumu
Mahiza amebainisha kuwa Rais ameamua kuanza ziara yake hiyo Wilayani Mafia
wilaya ambao mkoani humo ipo kisiwani na imekuwa ni ngumu watu wengi
kuitembelea mara kwa mara kutokana na jiografia yake kuwa ngumu na usafiri wake
ni wa shida kufuatia meli kushidwa kufika baada ya gati kuharibika.
Pia katika wilaya zingine Dkt Kikwete
ataweka mawe ya msingi na kuzindua miradi ya maendeleo kwenye sekta za Elimu,
Afya, Viwanda, Uchukuzi, Mawasiliano, Mahakama, Maji, Nishati na shughuli za
vijana.
Mkuu huyo ameongeza kuwa wakati wa
ziara hiyo wananchi watapata fursa ya kuzungumza na rais kupitia katika
mikutano ya hadhara iliyopangwa kila wilaya na kwamba majumuisho ya ziara yake
itafanyika wilayani Bagamoyo Oktoba 9
Ametoa wito kwa wananchi mkoani humo
kushiriki katika mapokezi ya rais na kuhudhuria kwa wingi kwenye mikutano ya
hadhara na kuhakikisha amani na utulivu unakuwepo wakati wote wa mikutano hiyo.
0 comments:
Post a Comment