Home » » Kituo kuwaenzi waasisi wa Taifa kujengwa Bagamoyo

Kituo kuwaenzi waasisi wa Taifa kujengwa Bagamoyo

Serikali imetunga sheria maalumu ya kuwaenzi waasisi wa Taifa ikiwamo kuanza ujenzi wa kituo cha kuwaenzi waasisi hao katika eneo la Kiromo, wilayani Bagamoyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani, aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kuadhimisha miaka 14 ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Kombani alisema tayari upembuzi yakinifu na athari za kimazingira umeshafanyika katika eneo hilo.

Alisema serikali pia imeshafanikiwa kuzitambua Taasisi na asasi zinazomiliki kumbukumbu, mali na vitu vyenye umuhimu wa kihistoria kitaifa ili kuvitunza vizuri.
Alisema kituo hicho kitakusanya na kuhifadhi kumbukumbu, mali na vitu vyenye umuhimu kihistoria vya waasisi hao kama ilivyoelekezwa katika sheria.

Waziri huyo alisema kituo hicho pia kitaratibu shughuli zote zinazohusu waasisi ikiwamo kuhamasisha umma kuhusu utafiti, kuandaa machapisho mbalimbali yanayoelezea michango na kazi walizowahi kuzifanya waasisi hao.

Aidha, alisema serikali imeshaunda Bodi ya Udhamini ya Mfuko wa kuwaenzi Waasisi wa Taifa ambayo itakuwa na jukumu la kutafuta, kukusanya na kusimamia mfuko huo.

Akizungumza katika mkutano huo, Balozi mstaafu Job Lusinde, alisema Mwalimu Nyerere alikuwa ni taasisi pekee kwa mchango wa maisha yake na mafundisho yake yalikuwa mchango mkubwa katika kujenga na kuimarisha umoja na uzalendo.

Lusinde alisema Mwalimu alikuwa mwanasiasa mwenye kipaji cha pekee na aliamini kuwa siasa kwake ni kuwatumikia watu waliompa dhamana ya kuongoza.

Alisema enzi za uongozi wake, Mwalimu Nyerere hakuwa na mchezo na mtu yeyote katika mambo ya msingi yenye maslahi mapana kwa Taifa.

 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa