Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani
linamshikilia Bahati Andulile maarufu kama Ester umri miaka 18 mfanya
kazi wa ndani kwa Bw. Alan Mziray kwa kosa la mauaji ya mtoto wa bosi
wake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Kamishina Msaidizi Ulrich Matei amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na ameeleza kuwa mwili wa marehemu aitwaye Arafat Alan umri miaka 3 na miezi 4 ulikutwa kwenye dimbwi la maji machafu katika eneo la kiwanja cha mpira Maili Moja majira ya saa 07:20 asubuhi Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani.
Kamanda Matei ameongeza kuwa mfanyakazi huyo wa ndani kwa Bw. Alan aliondoka na mtoto huyo tangu tarehe 06/10/2013 majira ya saa 4.00 asubuhi baada ya kutumwa kwenda sokoni kununua mahitaji lakini hakurudi tena na mtoto huyo hadi mwili wake ulipokutwa kwenye dimbwi la maji machafu akiwa amekufa.
Mwili wa marehemu baada ya kufanyiwa uchunguzi na Daktari ulikutwa ukiwa na majeraha Kichwani eneo la utosini na baada ya kumhoji msichana huyo amekiri kuhusika kwa tukio hilo na kudai kuwa alimpiga na kitu kizito utosini mtoto huyo.
Mtuhumiwa huyo ameeleza kuwa sababu za kumuua marehemu ni kutokana na yeye kuwa mgeni wa eneo ambalo alikuwa akifanya kazi na baada ya kupotea njia ya kurudi nyumbani, na kulala porini na mtoto huyo lakini kutokana na mtoto huyo kuwa analia aliona akimkera na kuamua kumpiga kwa kutumia kipande cha gongo kichwani.
Mwili wa mtoto huyo ulibainika na mpita njia na baada ya taarifa kufikishwa katika kituo cha Polisi Mtuhumiwa alikamatwa tarehe 08/10/2013 katika eneo la stendi Mailimoja akiomba usafiri wa kwenda nyumbani kwao Mbeya.
Katika tukio jingine, wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ally Hassan Mwinyi iliyopo Kata ya Kiromo Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani wamenusurika kupoteza maisha baada ya bweni la wasichana wa shule hiyo kuteketea kwa moto.
Bweni hilo lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi wa kike 81 ambalo walikuwa wakiishi wanafunzi wa kidatu cha kwanza na cha nne liitwalo Charles Omjoni liliteketea kwa moto saa 22:15 usiku wakati wanafunzi hao wakiwa wapo madarasani wakijisomea na kuteketeza vitu vyote vilivyomo humo ndani ambavyo bado thamani ya mali hiyo kujulikana.
Tukio hili ni la pili kutokea katika shule hiyo ndani ya siku tatu ambapo bweni lingine la shule hiyo liliteketea kwa moto na kusababisha wanafunzi 46 kupoteza mali zao wakati wakiwa wanajisomea usiku.
Kufuatia tukio hilo Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linawashikilia wanafunzi wanne kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani amewataja wanafunzi wanaoshikiliwa na Jeshi hilo kuwa ni Vanesa Godbles umri miaka 17 mwanafunzi wa kidato cha tatu, Lubna Adam umri miaka 15, mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Diana Ngita umri miaka 17 mwanafunzi wa kidato cha tatu, pamoja na Nawal Fabid umri miaka 14 mwanafunzi wa kidato kidato cha pili.
Aidha Kamanda Matei amethibitisha kupoteza maisha kwa Mbawala Salumu umri miaka 60 mkazi wa Vianzi Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani.
Kamanda Matei amewaeleza waandishi wa habari kuwa tukio hilo limetokea huko Vianzi Wilaya ya Mkuranga majira ya saa 17:30 jioni baada ya marehemu kujaribu kuzima moto uliokuwa unawaka kwenye shamba lake ndipo moto huo ulimzidi na kuzingira shamba hilo hali ilopeleka kifo chake.
Pia Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linamshikilia Mohamed Mustapha umri 30, baada ya kukutwa na noti bandia zenya thamani ya Tshs. 640,000/= .
Mtuhumiwa alikamtwa majira ya saa 22:00 usiku huko Kijiji cha Chole Wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani wakati akiwa dukani kwa Shumbuo Mlale kununua mahitaji yake na ndipo muuzaji wa duka hilo alimtilia mashaka noti alizotoa kumpatia.
Baada ya taarifa kuzifikia Jeshi la Polisi Mtuhumiwa huyo alikamatwa na kuhojiwa na kukutwa akiwa na noti 64 ambazo alikuwa amehifadhi kwenye bahasha na alieleza kuwa noti hizo alizipata baada ya kuuza magunia yake 62 ya mkaa kwa tajiri mmoja ambaye hamjui jina kutoka jijini Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment