KAMPUNI ya Agro Forest Plantation, mwishoni mwa
mwezi huu inatarajia kuanza kupanda mbegu za miwa zitakazotumika kwenye
mashamba mbalimbali mkoani Pwani.
Uamuzi huo umetokana na ombi lililotolewa na
wenyeviti wa vijiji vya Kata ya Chumbi wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani
walioitaka kampuni hiyo kuwekeza kwenye ardhi waliyowapa kwa ajili ya
uwekezaji.
Akizugumza jijini Dar es Salaam, mmoja wa
wakurugenzi katika Kampuni ya Agro Forest Plantation, Otieno Chaulo alisema
wameshawaleta wataalamu waliobobea katika mashamba ya miwa pamoja na viwanda
vya kutengeneza sukari.
Alibainisha kuwa wataalamu hao wanatoka nchini
India na wameshatembelea eneo la mradi lililopo Rufiji na wamependekeza aina ya
mbegu zitakazopandwa ambazo zitahimili udongo na hali ya hewa.
Aliongeza kuwa wataalamu hao watatu wamegawana
katika makundi matatu, mmoja akiwa na uzoefu katika kutambua aina ya mbegu
zitakazotoa sukari nyingi.
Otieno alisema mtaalamu mwingine ana ujuzi wa
kutambua na kutibu miwa na wa mwisho ni mtaalamu wa ujenzi wa viwanda.
Alibainisha kuwa wataalamu hao wameshatoa
mapendekezo ambayo yamekubaliwa na mwekezaji ambaye ni Agro Forest Plantation
kwa ajili ya utekelezaji. Pia wametoa ushauri kwa serikali kusaidia kupeleka
karibu miundombinu ya umeme pamoja na kuchonga barabara za mashamba ya wakulima
wadogo wadogo wanaozunguka mashamba hayo.
Otieno pia alisema baada ya kupandikiza mbegu
katika shamba la heka 500 mwishoni mwa mwezi huu, itachukua miezi 14 kustawi na
kuotesha katika shamba la kuanzia heka 4,000 ambazo zitaweza kutoa miwa kwa
ajili ya uzalishaji sukari.
Awamu ya kwanza ya uzalishaji sukari ambapo kiwanda
kitategemea kuanza Oktoba 2015 ni tani 1,500 na kuendelea miaka inayofuata hadi
kufikia tani 5,000 kama uwezo wake uliotathiminiwa katika uzalishaji sukari
katika bonde hilo la Rufiji.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment