Mke
wa Rais Mama Salma Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa Taasisi ya
Wanawake na Maendeleo (WAMA) akizungumza hivi karibuni na wanafunzi wa
Shule ya Sekondari Msimbu iliyopo wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani juu
ya umuhimu wa elimu na athari za mimba za utotoni wakati alipowatembelea
wanafunzi hao.
Mkuu
wa wilaya ya Kisarawe Bi.Fatuma Kimario akisisitiza jambo wakati Mke wa
Rais Mama Salma Kikwete alipotembelea Shule ya Sekondari Msimbu na
kuzungumza na wanafunzi wa shule hiyo ambapo aliwaasa wapende shule na
kuepukana na mambo mabaya kama vile mafataki na uvutaji bangi ili waweze
kufikia malengo waliojiwekea,kushoto ni Mke wa Rais Mama Salma Kikwete
ambaye pia ni mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo(WAMA)
anayefuatia ni Mwenyekiti wa Halmashauri Adam Ng’imba na kulia ni
Mwenyekiti wa CCM Kisarawe Bi.Tatu Kano. Picha na Lorietha
Laurence-Maelezo
******************************************
Na Anna Nkinda – Maelezo
Mke
wa Rais Mama Salma Kikwete amewataka wanafunzi wa kike kujiepusha na
mafataki ambao watawarubuni kwa vitu mbalimbali na hatimaye kuwapatia
ujauzito na ugonjwa wa Ukimwi na hivyo kutofikia malengo waliyojiwekea
katika maisha yao.
Pia
amewataka wanafunzi wa kiume kuachana na tabia ya kuvaa suruali
milegezo na uvutaji wa sigara ambao utawasababishia kupata ugonjwa wa
kansa ya koo na mapafu.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA) ameutoa wito huo hivi karibuni wakati akiongea na wanafunzi wa
shule ya Sekondari ya Msimbu iliyopo kata ya Msimbu wilaya ya
Kisarawe mkoani Pwani.
“Kama
wazazi wenu hawawasimanii kufuatilia mienendo yenu mjisimamie nyinyi
wenyewe kwa kukanyana na kutoa taarifa kwa walimu wenu pale ambapo
mtaona mwenzenu ana tabia ambazo ni kinyume na maadili ya
mwanafunzi kwa kufanya hivyo mtaepukana na tatizo la mimba za utotoni’,
alisema Mama Kikwete.
Kuhusiana
na madai ya wanafunzi hao kuwa wazazi wao wanakabiliwa na tatizo la
umaskini jambo ambalo linawafanya waweze kuingia katika vishawisi
mbalimbali Mama Kikwete alisema kuwa umaskini isiwe ni kigezo cha mtu
kufanya mambo yasiyofaa ili aweze kupata fedha jambo ambalo ni hatari
katika maisha yake.
“Ni
muhimu wazazi wakatafuta mbinu mbadala ya kuweza kukabiliana na hali
hii ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwani mtu akifanya kazi kwa bidii ni
lazima atafanikiwa na kuweza kupambana na hali ya umaskini kwani
atalima mazao na kuuza, atafanya biashara ndogondogo na kuweza kujipatia
kipato”, alisema Mama Kikwete.
Aidha
Mama Kikwete pia aliwataka wanafunzi hao kuitumia teknolojia vizuri
katika kujiletea maendeleo ikiwa ni pamoja na kujitafutia nyaraka za
kusoma “material” kwa ajili ya masomo yao na siyo tofauti kwani
teknolojia ikitumika vibaya ni rahisi mtu kuiga mambo ambayo ni tofauti
na utamaduni wake.
Akisoma
taarifa ya shule hiyo Mwalimu Mkuu Renatus Rweyemamu alisema kuwa tangu
shule hiyo ilipoanzishwa mwaka 2007 hadi sasa idadi ya wasichana
waliopata ujauzito ni 34 na wahusika wameshafikishwa kwenye vyombo vya
dola na hivi sasa suala hilo linasimamiwa na watendaji wa vijiji husika.
Alizitaja
changamoto zinazoikabili shule hiyo kuwa ni wanafunzi kutembea umbali
mrefu kufuata shule jambo ambalo linasababisha kuingia darasani wakiwa
wamechoka pia wasichana wanakutana na vishawishi vingi wakiwa njiani,
hosteli moja haitoshi kwa kuwa inauwezo wa kuchukua wanafunzi 48 pia
haina vitanda wala magodoro ya kulalia.
Mwalimu Rweyemamu
alisema, “Changamoto nyingine ni wazazi kutofuatilia kwa ukaribu
mienendo ya watoto wao pia kutokutoa ushirikiano wakati wa kuwafuatilia
wahusika waliowapatia ujauzito watoto wao”.
Aliiitaja
mikakati waliyojiwekea kuwa ni kufanya mikutano na wazazi ili kuwapa
ushauri jinsi gani wanaweza kufuatilia mienendo ya watoto wao na
kutafuta wafadhili watakaowasaidia kujenga Hosteli ikiwa ni pamoja na
kununua vitanda, magodoro na kuweka umeme jua.
“Pamoja
na majukumu mengi yanayokukabili ombi letu kubwa kwako kwa sasa ni
tunaomba kama itawezekana utununulie vitanda na magodoro kwa Hosteli
yetu”, alisema Rweyemamu.
Shule
ya Sekondari ya Msimbu ni shule ya kata ambayo inajumla ya wanafunzi
463 wasichana wakiwa ni 250 na wavulana 213 ambao wanatoka katika vijiji
sita vilivyopo katika kata ya Msimbu.
0 comments:
Post a Comment